TAHARIRI: Ushuru huu mpya utawaathiri wengi
Na MHARIRI
MWAKA mpya unapong’oa nanga, Mkenya anajipata katika njia panda kuhusiana na jinsi anavyoendelea kuchangia ustawi wa taifa lake.
Katika hatua ya punde zaidi ambayo huenda ikazidisha mambo kuwa magumu kwa wananchi, serikali kuanzia jana ilianza rasmi kutoza ushuru wamiliki wa biashara ndogo ndogo kama vinyozi, mama mboga na sekta ya Juakali ushuru wa moja kwa moja.
Ushuru huu unatozwa hata baada ya kuwa, tayari wananchi wanakabiliwa na hali ngumu za kiuchumi. Kuanzia Jumatatu, wazazi wanawarejesha watoto wao shuleni ambapo watahitajiwa kugharamikia sare, vitabu na hata karo kwa wanaosoma shule za kibinafsi, za upili na vyuoni.
Sasa itakuwa lazima kwa kila mfanyibiashara mdogo kulipa ushuru wa asilimia tatu kwa mauzo ya kila mwaka.
Ingawa haijafahamika vigezo ambavyo Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) itatumia kupima mauzo hayo, ushuru huo unajiri serikali inapoanza kulipa deni ya kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi.
Kufikia mwishoni mwa mwaka jana, Kenya ilikuwa na deni la Sh6 trilioni kutoka mashirika mbalimbali ya kifedha ulimwenguni na ya humu nchini.
Hii ina maana kuwa huenda bidhaa na huduma katika sekta ya jua kali zitapanda kutokana na ushuru huu mpya, unaotokana na sheria ya fedha ya 2019 ambayo Rais Uhuru Kenyatta aliidhinisha mwaka jana.
Tayari mazingira ya kufanya biashara Kenya yamekuwa yakidorora kutokana na sera za serikali. Uamuzi huu ni kinyume na mipango ya awali ya seriikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kutoa nafasi 500,000 za kazi kila mwaka.
Katika majukwa mbalimbali, serikali inaendelea kunadi kuhusu mpango wa kuendeleza Ajenda Nne Kuu za ustawi. Uzalishaji Chakula cha Kutosha, Kupatikana Nyumba za bei nafuu, Huduma za Afya kwa wote na Ustawishaji Viwanda ni mambo yanayohitaji mazingira ambapo kuna wananchi wanaojimudu kimaisha.
Hata serikali izalishe mabilioni ya tani za chakula au inunue dawa na kuweka vifaa vya kisasa hospitalini, bado kutakuwa na uhaba kwa kuwa kila mtu atakuwa anahitaji usaidizi. Si vibaya kwa serikali yoyote kuwatoza ushuru raia wake, lakini ushuru huo yafaa uwanufaiishe raia hao. Huu wa kulipia deni utawaathiri wengi.