Makala

TAHARIRI: Usiri wa wananchi wafaa kuheshimiwa

February 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Mwanamume akitumia simu yake. Serikali haifai kumruhusu mtu yeyote kuingilia usiri wa mwengine. Hii ni haki ya kuzaliwa ambayo haifai kukiukwa bila ya sababu maalumu. Sheria hiyo yafaa kutekelezwa kwa uangalifu mkubwa, ili isiturudishe nyuma. Picha/ Hisani

Na MHARIRI WA GAZETI LA TAIFA LEO

Kwa Muhtasari:

  • Watu wamekuwa wakiwahangaisha wenzao kwenye mitandao na kuwaibia mali ya mamilioni
  • Mahabusu na wafungwa magerezani pia wamekuwa wakiendeleza ukora mtandaoni
  • Serikali inapanga kuwatumia polisi kunusa na kufuatilia kwa makini mawasiliano ya wananchi
  • Haki ya usiri imo kwenye Katiba yetu na hakuna sheria inayoruhusu mtu yeyote kuingilia usiri wa mwengine

KILA Mkenya ana haki ya kulindwa dhidi ya kuvamiwa na watu wenye nia mbaya, hasa mitandaoni.

Kumekuwa na visa vya watu kuwahangaisha wenzao kwenye mitandao, na hata wakati mwingine kuendeleza uhalifu wa kusababisha wizi wa mali ya mamilioni.

Wahalifu wakiwemo magaidi wamekuwa wakipanga njama za kutekeleza mashambulizi kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook. Baadhi ya makundi ya watu yanakuwa na majina ya kuonyesha labda ni wafanyibiashara wa kawaida, lakini huwa na malengo fiche ambayo yanaweza kuwadhuru wananchi.

 

Ukora

Mahabusu na wafungwa magerezani pia wamekuwa wakiendeleza ukora kupitia vifaa vya kielektroniki kama vile simu.

Kwa hivyo serikali yoyote inayojali watu wake, haina budi kuja na mbinu za kuhakikisha kuwa, yeyote anayeingia mitandaoni atakuwa salama. Mswada wa Cyber Crimes Bill unalenga kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo, na hilo ni jambo zuri.

Hata hivyo, katika kutekeleza sheria hiyo, serikali inapanga kuwatumia polisi kunusa na kufuatilia kwa makini mawasiliano ya wananchi. Mawasiliano hayo yatakuwa kupitia simu au mitandao ya kijamii.

Polisi watapewa nguvu za kusikiza na hata kurekodi mazungumzo binafsi baina ya watu, hata wasiokuwa na nia yoyote mbaya.

 

Kumaliza uwazi

Haijalishi ni sababu zipi za msingi zitakazotumiwa, inavyofahamika ni kuwa polisi wana mazoea ya kujichukulia sheria mikononi. Iwapo wataruhusiwa kisheria kuchunguza, watakuwa wakihangaisha watu na kufanya iwe vigumu kwa wananchi kuzungumza kwa uwazi.

Pia, badala ya wananchi kufichua wahalifu, watakuwa wakizungumza kwa tahadhari kwa kuhofia kutambuliwa. Kwa sababu ya sifa za ufisadi zinazohusishwa na polisi, iwapo katika kusikiza mazungumzo ya watu watasikia habari kuwahusu wahalifu, kuna uwezekano wawaeleze na mapema. Hilo litafanya iwe vigumu mno kuangamiza uhalifu nchini.

Jambo hili mwaka 2017 lilipingwa vikali na wananchi, na hata kampuni za mawasiliano kama vile Safaricom.

Haki ya usiri imo kwenye Katiba yetu na hakuna sheria inayoruhusu mtu yeyote kuingilia usiri wa mwengine. Hii ni haki ya kuzaliwa ambayo haifai kukiukwa bila ya sababu maalumu. Sheria hiyo yafaa kutekelezwa kwa uangalifu mkubwa, ili isiturudishe nyuma.