TAHARIRI: Uteuzi serikalini uzingatie uwazi
NA MHARIRI
HATUA ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) Joe Mucheru kubatilisha uteuzi wa Bw Jared Peter Odoyo Kwaga kama mwanachama wa baraza la Taasisi ya Mafunzo ya Uanahabari Kenya (KIMC) inapaswa kupongezwa.
Bw Mucheru aliondoa jina la Bw Kwaga ilipoibuka kuwa ni mmoja wa washukiwa ambao wameshtakiwa katika kesi inayohusu kupotea kwa Sh2 bilioni katika kaunti ya Migori.
Kwa kuchukua hatua hiyo, Bw Mucheru ameonyesha sifa ya kiongozi anayejali hisia za wananchi, ila inazua maswali kuhusu vigezo vijavyozingatiwa katika teuzi za watu maarufu kuhudumu katika mashirika mbalimbali ya serikali.
Hili pia lilijitokeza kwenye teuzi za wakuu wa mashirika mbalimbali ya serikali, ambazo Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri walifanya mwishoni mwa wiki iliyopita.
Karibu watu wote walioteuliwa ni wanasiasa walioshindwa kwenye chaguzi zilizopita, huku wengi wao wakiwa hawana ujuzi wala tajriba ya kusimamia baadhi ya asasi walizoteuliwa kuhudumu.
Kuna maswali yanayoibuka: Je, teuzi hizo zilipigwa msasa kabla ya kutangazwa? Kando na umuhimu wao wa kisiasa, ni vigezo vipi vilivyozingatiwa katika teuzi zao?
Haya yanaibuka ikizingatiwa kwamba kabla ya kuajiriwa, Wakenya huhitajika kutoa vyeti vingi kuonyesha kwamba wamehitimu kuhudumu katika nafasi wanazoomba kazi.
Baadhi ya stakabadhi hizo ni cheti kutoka kwa Idara ya Polisi kuonyesha hawana rekodi yoyote ya uhalifu, Halmashauri ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kuonyesha wamemaliza kulipa mikopo yao, Halmashauri ya Kutathmini Madeni (CRB), Halmashauri ya Kukusanya Ushuru (KRA) kati ya vingine.
Kilicho wazi ni kwamba wengi ambao hukosa vyeti hivyo huachwa nje kwa kisingizio cha “kutotimiza kanuni zilizowekwa.”
Hili hutamausha wengi kwani taratibu za kupata vyeti hivyo pia huwa ndefu na zinazomgharimu mtu pesa.
Kwa kufahamu uhalisia huu, imefikia wakati serikali kuanza kuzingatia uwazi katika teuzi muhimu zinazohusu usimamizi wa asasi zake muhimu.
Ni kinaya kwa wanasiasa waliokataliwa na wananchi kuteuliwa kuhudumu katika mashirika hayo, huku maelfu ya vijana wakihangaika nchini bila nafasi za ajira.