TAHARIRI: Uteuzi wa Amina kuinua spoti nchini
Na MHARIRI
HALI ya mchezo wowote inaweza kuimarika ikiwa viongozi wake watajitahidi kusaidia mipango ya kuinua sekta hiyo.
Usimamizi wa michezo mbalimbali ya humu nchini unahitaji watu walio tayari kujitolea kwa lengo la kuhakikisha kwamba Kenya inafikia viwango sawa na vile vya mataifa mengine.
Wizara ya Michezo nchini imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi katika miaka ya hivi karibuni kwa sababu ya uongozi mbaya usiojali mahitaji ya wanamichezo wala kushughulikia ipasavyo suala la kuwepo kwa vifaa na viwanja.
Kwa akali kubwa, kutofaulu kwa sekta ya michezo nchini Kenya kunaweza kuhusishwa na ukosefu wa utaalamu miongoni mwa viongozi wanaoteuliwa kuisimamia sekta hiyo.
Hata hivyo, uteuzi wa Dkt Amina Mohamed kuwa Waziri wa Michezo unatazamiwa kuamsha upya ari ya kuthaminiwa kwa michezo kinyume na jinsi hali imekuwa katika miaka ya nyuma chini ya watangulizi wake.
Akiwa Waziri wa Masuala ya Kigeni, Dkt Amina alifaulu zaidi kuinyoosha idara hiyo.
Utendakazi wake hata katika Wizara ya Elimu uliaminiwa pakubwa na Wakenya wengi.
Hapana shaka kwamba uzoefu alionao pamoja na tajriba yake ni miongon mwa sifa zilizozingatiwa na Rais kabla ya kumpokeza Dkt Amina mikoba ya Wizara ya Michezo.
Licha ya changamoto za kila aina ambazo kwa sasa zinaikumba sekta ya michezo humu nchini, Wakenya wana kila sababu ya kujijengea matumaini tele kufuatia uteuzi wa Amina.
Waziri Amina anashika hatamu katika kipindi muhimu zaidi kwenye historia ya sekta ya michezo humu nchini. Kikosi cha kitaifa cha soka Harambee Stars kwa sasa kinajiandaa kushiriki fainali za kuwania ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri kati ya Juni na Julai 2019.
Matarajio ya kila Mkenya ni kwamba chini ya Dkt Amina, Stars itafaulu kutinga hatua ya robo-fainali, haya yakiwa pia malengo ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Bw Nick Mwendwa.
Tangu mapambano ya AFCON yaanzishwe, Kenya iliyofuzu kwa kivumbi hicho kwa mara ya mwisho mnamo 2004, haijawahi kupita hatua ya makundi.
Baruapepe: [email protected]