Makala

TAHARIRI: Wadau waungane kudhibiti maambukizi ya HIV

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KUIBUKA kwa ripoti kuwa maambukizi ya virusi vya HIV yameongezeka nchini kutokana na migomo ya mara kwa mara ya wahudumu wa afya kunatamausha.

Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Maradhi ya Ukimwi (NACC), laonyesha maambukizi kutoka wa akina mama hadi kwa watoto yameongezeka kutoka asilimia nane hadi 11.

Akina mama wengi hukosa huduma muhimu wanapojifungua, wahudumu wakiwa katika migomo wakishinikiza kuongezwa mishahara yao. Hilo limechagia wengi wao kuwaambukiza wana wao.

Kimsingi, hizi ni habari za kusikitisha kwani zinatokea wakati Kenya inaweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya afya.

Vile vile, ni sikitiko kuu kwani zinatokea wakati nchi nyingi duniani zimepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi hayo kutokana na kuimarika kwa teknolojia za utoaji matibabu.

Hii inapaswa kuwa changamoto kuu kwa wadau wote muhimu, hasa katika serikali kuu, kufahamu kuhusu athari za migomo ya mara kwa mara ya wauguzi na madaktari.

Ni dhahiri kuwa sekta ya afya imekumbwa na msururu wa changamoto tangu usimamizi wake kukabidhiwa serikali za kaunti.

Kinyume na awali, ambapo migomo ya wahudumu haingesikika, hali imekuwa tofauti.

Wananchi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa dawa, dhuluma kutoka kwa baadhi ya wahudumu, kupewa dawa zisizofaa kati ya malalamishi mengine.

Serikali za kaunti nazo zimekuwa zikitishia kuwaadhibu wahudumu ambao hushiriki katika migomo.

Baadhi yao huwa wanaadhibiwa vikali ama kufutwa kazi bila taratibu zifaazo kuzingatiwa.

Isitoshe, wengi wao hupokea mishahara duni, huku wakati mwingine ikichelewa kwa miezi.

Hili huwatamausha wengi, hali ambayo huchangia kudorora kwa huduma za matibabu wanazotoa kwa wananchi.

Kutokana na hayo, wito wetu ni wadau wote wa afya kuungana ili kuimarisha huduma katika hospitali za umma.

Ni makosa kwa ulegevu wa baadhi ya wahudumu kuchangia mtoto asiye na hatia kuambukizwa virusi hatari, ambavyo humwathiri katika uhai wake wote duniani. Hatia ya mtoto ni ipi?

Imefikia wakati wadau wote wanapaswa kutilia maanani maisha ya watoto hao, hata wanapotetea kuimarishwa kwa maslahi yao.