Makala

TAHARIRI: Wimbi la mwamko Ukraine lisipuuzwe

April 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

WAPIGAKURA milioni 13 nchini Ukraine walikubaliana kwa kauli moja siku ya Jumapili kumchagua mcheshi Volodymyr Zelensky kuwa rais wao.

Zelensky ambaye tunaweza kumfananisha na mwanahabari Walter Mong’are (Nyambane) alivyokuwa akimuigiza Rais mstaafu Daniel arap Moi, alipata asilimia 73 ya kura kwenye marudio ya uchaguzi.

Ingawa hakueleza wapiga kura 35 milioni waliosajiliwa, jinsi anavyopanga kuongoza nchi akiwa rais, Bw Zelensky alivutia wengi kwa ujumbe wake kuhusu uovu wa ufisadi uliokithiri.

Alipata umaarufu kwa kuigiza kwenye televisheni akiwa rais. Kwenye mzaha wake, alikuwa akionyesha namna ufisadi ulivyoirudisha nyuma Ukraine.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa jijini Kyiv wanasema japokuwa Zelensky hana uzoevu wowote wa uongozi wala hajasema anavyopanga kuendeleza nchi hiyo, raia wanaamini alikuwa chaguo bora kuliko wenzake 38 ambao sira ni zile zile.

Uamuzi huo wa watu wa Ukraine unatoa taswira kamili kwa viongozi wa Afrika ambao wameshindwa kabisa kukabiliana na ufisadi.

Hapa Kenya, wananchi wamefika hatua ya mwisho ya uvumilivu dhidi ya jinamizi hili, ambalo linawanyima maendeleo.

Ufisadi umekita mizizi katika karibu kila taasisi ya umma. Hata katika afisi za serikali, unapotaka jambo lifanywe kwa haraka huna budi kutoa ‘kitu kidogo’.

Kwa mfano katika afisi za usili wa vyetiu vya kuzaliwa, vitambulisho na pasipoti, watu wenye pesa huharakishiwa mambo huku wale wasiokuwa tayari wakicheleweshewa stakabadhi hizo, wakati mwingine kwa miezi.

Ufisadi Kenya umefanya vijana wengi wajiulize kwa nini wasome kwa bidi ilhali wanapopita mitihani wakiwa na vyeti vizuri, watahangaika kwa miaka kutafuta ajira au biashara za kufanya kutokana na mifumo ya ufisadi kuwafungia milango.

Mwamko uliopo Kenya kwa sasa ni wa hali ya juu kiasi kwamba hata watoto wa shule za msingi wanaelewa kuwa ufisadi ndio kikwazo kwa maendeleo ya Kenya.

Hali hii yafaa kuwatia baridi wanasiasa waliopo uongozini, ambao wanatumia muda wao mwingi wakizozana hadharani, badala ya kutatua tatizo halisi linaloikumba nchi.

Iwapo kufikia 2022 serikali ya sasa na viongozi wa Upinzani hawatakuwa wamebadilisha hali ya maisha ya mwananchi, haitakuwa ajabu watu wakiamua kuchukua mkondo wa wenzao wa Ukraine.