Makala

Talaka chafu wandani wakigeuka mahasimu

Na JUSTUS OCHIENG October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WALIKAIDI vizingiti vyote na kuungana kwenye uchaguzi wa urais 2022, wakashinda na kuingia mamlakani.

Hata hivyo, sasa ni rasmi kwamba uhusiano kati ya Rais William Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua, huenda hautawahi kuwa ulivyokuwa tena, aondolewe mamlakani au aokolewe na seneti au mahakama.

Huku akitiwa nguvu na uhusiano wake mpya na aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa 2022, Raila Odinga, Rais Ruto, ingawa bado hajatoa taarifa kwa umma kuhusiana na hoja ya kumng’oa mamlakani naibu wake, anaonekana kuiunga kikamilifu.

Hili linadhihirika kutokana na kuungwa kwa hoja hiyo na wabunge wengi kutoka chama chake cha United Democratic Alliance (UDA), na Orange Democratic Movement (ODM) cha Bw Odinga.

Wabunge 282 walipiga kura ya kumtimua ofisini Bw Gachagua katika hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.

Hata hivyo, bila kujali matokeo ya hoja hiyo katika seneti, wadadisi wanasema, uhusiano wa Rais Ruto na Bw Gachagua umeharibika kiasi cha kutorekebishwa.

Mbunge wa Tharaka, George Murugara alisema kwa kumuondoa mamlakani Bw Gachagua, Bunge lilikuwa linaheshimu tu matakwa ya watu waliotaka aondolewe kupitia ushiriki wa umma.

‘Iwapo atanusurika atafanya kazi wapi? Hawezi kufanya kazi na rais kwa sababu alisema hoja hii inafadhiliwa na rais. Hatukuwa na mkutano wa kundi la wabunge wa kuchukua msimamo wa pamoja,’ alisema Bw Murugara.

Washirika wa Bw Gachagua tayari wameahidi mapambano makali dhidi ya Rais William Ruto iwapo naibu rais atatimuliwa afisini.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alitaja hatua ya kumtimua Bw Gachagua kuwa dharau kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

‘Bado tunamwambia rais kwamba ana fursa ya kurudisha umaarufu wake mlimani na kuokoa hali lakini hakuna mtu anayepaswa kumdaganya kuwa hali ni kama zamani.

‘Lakini tunataka kusema kwamba, mashtaka ya kuondolewa kwa Gachagua ni ya kipuuzi sana na hoja kama hiyo ni shambulio dhidi ya watu wa eneo la Mlima Kenya na yana madhara makubwa kwa nchi,’ Bw Kahiga alisema.

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi aliambia Taifa Leo kuwa, uhusiano kati ya Rais Ruto na naibu wake unaonekana kuvunjika kiasi cha kutorekebishwa.

‘Uhusiano wa viongozi hao wawili hauwezi kamwe kuwa sawa, huku ukijua vyema mwenzako ndiye anayechochea kukuondoa afisini,’ Bw Mwangangi alisema.

Bw Gachagua, ambaye uhusiano wake na bosi wake umedorora sasa amewasilisha kesi mbalimbali kortini ili kujinusuru dhidi ya kung’olewa madarakani, huku rais akiendelea kunyamaza.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anahoji kuwa, kutokana na jinsi wandani wa Rais Ruto walivyoshughulikia hoja ya kumuondoa mamlakani, uhusiano kati ya Naibu Rais na bosi wake yamkini ‘umevunjika kiasi cha kutorekebishwa.’

‘Kwa matamshi yake ya kudharau, kumsuta rais na ushujaa wa kisiasa, Gachagua alivuka mipaka, na uhusiano wake na Ruto umevunjika kiwango cha kutorekebishwa,’ Bw Bigambo aliambia Taifa Leo mnamo Jumatatu.

Aliendelea: “Hakuna tena uaminifu na heshima kati yao. Gachagua alikosea kuchukulia ushawishi wake unaokua katika Mlima Kenya kama mtaji muhimu wa kisiasa, na ni wazi, uamuzi wake haukuwa sahihi.

Anaweza tu kupima ushawishi wake wa kisiasa kwa kujiuzulu na kukabiliana na Ruto katika uchaguzi, au kuvumilia atimuliwe na kusahau siasa kabisa.

Naibu kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Ayub Savula, aliambia Taifa Leo kwamba, kwa mtazamo wa mambo,’ Gachagua anaenda nyumbani,’ na hakuna uwezekano wa kupatana na bosi wake.

“Wabunge wengi wameamua kumtimua Gachagua na rais hawezi kuwashawishi vinginevyo na sioni Riggy G akibadilika hata kama atanusurika. Uhusiano wake na viongozi umedorora,” akasema.