TEKNOHAMA: Facebook kuzima habari feki za tiba
Na LEONARD ONYANGO
MITANDAO ya kijamii ni sawa na maji ya mafuriko; hubeba takataka na vitu vya thamani.
Licha ya mitandao ya kijamii kuwezesha watu kuwasiliana kwa urahisi, imesheheni habari tele za kupotosha.
Hivi majuzi serikali ya Amerika ilitangaza kuwa itatumia jeshi kukabiliana na habari za kupotosha huku ikisema kuwa taarifa hizo feki zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii zinatishia usalama wa nchi hiyo.
Wizara ya Ulinzi ilisema kuwa itatumia teknolojia ya kisasa itakayogundua habari za kupotosha zaidi ya 500,000 ambazo huchapishwa kwenye mitandao ya kijamii kupitia maandishi, picha na hata video kwa siku.
Habari feki hukolea zaidi uchaguzi unapokaribia karibu katika nchi zote ikiwemo Kenya.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa mamilioni ya taarifa za kupotosha kuhusu matibabu huchapishwa kila siku katika mitandao ya kijamii, haswa Facebook na Instagram.
Mitandao ya Facebook na Instagram wiki mbili zilizopita ilitangaza kuzindua programu ya kukabiliana na habari feki kuhusu chanjo mbalimbali.
Kampuni ya Facebook inayomiliki Instagram ilisema kuwa sasa kisanduku cha kuelimisha watumiaji wa mitandao hiyo ya kijamii kitajitokeza kila mara wanapotafuta taarifa kuhusu aina yoyote ya chanjo.
Kisanduku hicho cha kuelimisha watumiaji kitashauri watu kusoma taarifa za kweli katika tovuti za mashirika ambayo yanaaminika.
Kwa watumiaji kutoka Kenya, Facebook na Instagram, kitakusihi kupata taarifa sahihi kutoka tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Watumiaji wa mitandao hiyo kutoka Amerika watatakiwa kupata taarifa sahii kutoka tovuti ya Taasisi ya Kutafiti Maradhi (CDC).
Nchini Kenya, viongozi wa kidini wamelaumiwa kwa kueneza taarifa za kupotosha kuhusu chanjo.
Baadhi ya makanisa yamekuwa yakieneza madai kwamba baadhi ya chanjo zinalenga kupunguza idadi ya watu nchini kwa kuzuia watu kupata watoto.
Viongozi wa kidini pia wanatumia mitandao ya kijamii kuwashinikiza waumini wao kukataa chanjo.
Viongozi wa kisiasa pia wamelaumiwa kwa kuwa kiini cha habari za kupotosha kuhusu chanjo.
Mnamo 2017, kinara wa ODM Raila Odinga alidai kuwa chanjo ya pepopunda iliyotolewa na serikali ilisababisha wanawake zaidi ya 500,000 kukosa uwezo wa kuzaa.
Madai hayo ya Bw Odinga yalipeperushwa na kuchapishwa na vyombo vya habari huku wanablogu wakiyasambaza kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Taasisi za afya zimemiminia sifa tele Facebook kwa kuanzisha teknolojia ya kuwakinga watumiaji wake dhidi ya habari feki kuhusu matibabu.
“Wazazi wengine wamekuwa wakitumia mitandao kutafuta taarifa kuhusu chanjo kutoka kwa wazazi wenzao. Mara nyingi taarifa wanazopata mitandaoni huwa za kupotosha,” akasema msemaji wa CDC Kristen Nordlund.
“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukabiliana na taarifa za kupotosha kuhusu matibabu,” akaongezea.
Kukataa chanjo
Wataalamu wa matibabu wanasema kuwa taarifa feki zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zimesababisha watu wengi kukataa kupewa chanjo dhidi ya baadhi ya maradhi.
“Shirika la WHO limekuwa likifanya mazungumzo kwa miezi kadhaa na Facebook kuhusu jinsi ya kuwezesha watu kupata habari sahihi kuhusu chanjo,” akasema Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.
“Taarifa za kupotosha kuhusu chanjo ni hatari kwa afya na zinatishia hatua zilizopigwa katika kukabiliana na maradhi yanayoweza kuzuilika,” akaongezea.
Mtandao wa Youtube pia umeanza kuondoa matangazo yanayotoa taarifa za kupotosha kuhusu chanjo.
Kampuni Amazon wiki iliyopita, ilifuta video ya kupinga chanjo iliyokuwa imepakiwa katika mtandao wake.