NGILA: Teknolojia itaendelea kugeuza Krismasi, hivyo jiandaeni
Na FAUSTINE NGILA
Kuna wakati mwanzoni mwa karne ya 19 ambapo sikukuu ya Krismasi haikuwa inasherehekewa. Baadaye ilijizolea umaarufu kama sikukuu ya kila mwaka na kuenea katika mataifa mengi duniani.
Tangu wakati huo, tumejionea mageuzi hasa kutokana na ubunifu wa jinsi ya kuitambua siku hiyo, na sasa teknolojia imebadilisha mtazamo wa wanadamu kuhusu siku hiyo.
Hili lilinichochea kufikiria jinsi Krismasi ya siku za usoni itakavyokuwa, nikizingatia mageuzi ya kiteknolojia tunayoyaona kwa sasa.
Kwa sasa ni vyema wanadamu wote wazoee kununua zawadi na vifaa vya kusherehekea siku hii mitandaoni. Hii itakusaidia kukwepa msongamano wa magari na kung’ang’anIa maeneo ya maegesho katika maduka ya jumla.
Kutakuwa na magari ya kidijitali yanayojiendesha yenyewe kwa barabara zake tofauti, ambayo Wakristo wataweza kuyatumia kwenda kanisani au kuyatuma kupeleka zawadi.
Kadi za heri njema ya Krismasi tayari zimegeuzwa kuwa za kidijitali, huku video za salamu zikiwezesha watu kutoka mataifa mbalimbali kuwasiliana. Teknolojia pia imeimarisha utangamano wa familia katika msimu huu, huku teknolojia ya WhatsApp ikiwapa watu nafasi YA kuunda kundi la mtandaoni la kuwasiliana kupitia maandishi, picha na video mbashara.
Katika sherehe za usoni za Krismasi, utaziona roboti zikipikia Wakristo chakula na kuandaa vinywaji, huku nazo droni zikitumiwa kupeleka zawadi kwa watu uwapendao.
Kuhudhuria ibada ya Krismasi kanisani, Wakristo watazoeshwa teknolojia ya hologramu, ambayo huleta kila tukio la ibada hadi sebuleni, ambapo utatazama na pia kutoa sadaka.
Utazamaji wa nyimbo za ibada, mahubiri, maombi na pia kuwaona wenzako ni kana kwamba umo kanisani. Kwa sasa, Wakristo wanasoma vifungu vya Biblia katika simu zao, na hii inawawezesha kutembea nayo kila mahali.
Lakini licha ya teknolojia hizi zote, mawasiliano bora zaidi ni yale ya uso kwa macho kwani kuna mambo au hisia ambazo teknolojia haiwezi kufanya. Ukweli ni kwamba teknolojia na uvumbuzi huu huja kwa gharama, na si kila Mkristo ataweza kumudu bei yake. Katika mwongo unaoanza 2020, Wakristo watazidi kufurika makanisani kila tarehe 25 Desemba.
Hata hivyo, teknolojia itazidi kutumiwa makanisani, jiandae. Kwa sasa video za moja kwa moja kutoka kanisani zinaweza kutazamwa katika mtandao wa YouTube kote duniani.
Pia, wumini wengi wanamiliki simu za kisasa zitakazowawezesha kusoma kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Tumia teknolojia kumtukuza Maulana. Nakutakieni Krismasi Njema na Mwaka Mpya wenye fanaka.