Teknolojia: Mitambo ya kisasa wakulima kukabiliana na matapeli sokoni
MOJAWAPO ya changamoto kubwa zinazokumba wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini, hasa maeneo ya mashambani ni ukosefu wa soko la bidhaa zao.
Isitoshe, hawana miundomsingi au vifaa kuhifadhi maziwa hivyo basi kuwaongezea hasara bin hasara.
“Idadi kubwa hawana mashine wala mbinu za kisasa kuhifadhi maziwa yao kwa muda mrefu bila kuharibika,” asema John Arusei.
Arusei ni mwenyekiti wa Bronjo Dairy Farmers Cooperative Society, muungano wa wakulima wa maziwa kutoka eneo la Bronjoviungani mwa mji wa Eldoret.
Kwenye mahojiano ya kipekee, aliambia Akilimali Dijitali kwa sababu hiyo mabroka na wachuuzi tapeli wamekuwa wakitumia fursa hiyo kupunja wakulima.
Kwa upande mwingine, wateja wengi bado wanaishia kununua maziwa yaliyochakachuliwa kwa maji au mchanganyiko wa vitu vingine bila kujua.
Kulingana na Arusei, ufaafu wa mitambo ya kisasa umekuwa mhimili mkubwa kwao kufanikisha biashara ya maziwa ndani na nje ya Kaunti ya Uasin Gishu.
Sio tu kujiongezea kipato, bali pia kuepuka hasara kwa kuzuia upotevu wa maziwa pale yanapokosa soko.
Pia, anaungama kwamba gharama ya kulisha mifugo imepanda lakini bado mabroka wananunua maziwa kwa bei ya chini.
Mwaka uliopita, 2023, ripoti ya Wizara ya Kilimo ilionyesha kuwa Kenya ilizalisha lita bilioni 4.2 Za maziwa kinyume na uwezo wake wa kuzalisha lita bilioni 12.
Hii ikiashiria kwamba endapo wakulima zaidi kutoka mashinani watafikiwa na teknolojia za kisasa katika sekta ya maziwa, wanaweza kuzalisha hata zaidi ya maradufu ya lita za maziwa zinazolengwa.
Kwa kawaida, mashinani maziwa hununuliwa kati ya Sh35 na Sh40 kwa lita.
Kwa sababu ya kukosa majokofu, Arusei anasema wakulima wengi vilevile wamekuwa wakilazimika kumwaga maziwa kwa sababu ya kukosa wanunuzi jambo linalofanya wengi wao kutumbukia kwenye lindi la umaskini.
Lakini kupitia teknolojia na bunifu za kisasa, wanaweza kujifunza kutengeneza bidhaa kama vile siagi, maziwa ya mtindi (yoghurt) ili wajiongezee kipato na pia waepuke kero ya mabroka.
Kwa sababu hiyo, Akilimali Dijitali imebaini kwamba wakulima wa Bronjo Dairy Cooperative Societies wanamiliki baadhi ya mtambo wa kiteknolojia ya kisasa kuhifadhi maziwa.
Mtambo huu ambao unaweza kuhifadhi zaidi ya lita 1, 000 za maziwa, kwa asilimia kubwa umesaidia kuhifadhi lita nyingi za maziwa ambayo huchukuliwa kila baada ya siku tatu.
Hii ni habari njema kwa wakulima ambao walikuwa wamezoea kuyachuuza maziwa yao kwa bei duni barabarani.
Kwa upande mwingine, mtambo huu umesaidia wakulima kudumisha usafi wa maziwa yao kwani hupitia hatua nyingi kabla ya kuhifadhiwa ndani ya coolers.
Mbali na hayo, wamepiga hatua na kumiliki mtambo maalum wa kupima kiwango cha maji kwenye maziwa na mizani ya kupima kilo au lita za maziwa ambazo mkulima atakuwa amezileta
Kwingineko, Elkana Tenai ambaye ni mkulima anasema teknolojia hiyo imekuwa ikiwasaidia kudumisha maziwa yao kwa muda mrefu.
Isitoshe, huwapatia muda wa kukusanya maziwa kwa wingi kutoka vijiji jirani.
Licha ya changamoto za mara kwa mara kulipia umeme na mtambo wenyewe kuharibika, anaomba serikali kuu kupitia Wizara ya Kilimo na serikali za ugatuzi kuwekeza kwa wakulima wadogo vijijini.
Ni hatua ambayo itasaidia kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana na pia kuwaongezea kipato wakulima ambao wanategemea ufugaji wa ng’ombe