MakalaMaoni

MAONI: Trump anaendelea kuvuruga mambo Amerika na Afrika

Na DOUGLAS MUTUA March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KUMEKUCHA Amerika! Mabalozi wanafukuzwa. Vituo vya redio vilivyoanzishwa miaka ya arobaini vinafungwa.

Wafanyakazi wa serikali wanafutwa bila ilani.

Hiyo ndiyo Amerika mpya ya Donald J. Trump.

Wasemao husema siku njema huonekana asubuhi, lakini hii ni aljafiri ya muhula wa pili wa utawala wa Trump, kwa hivyo bado tuna miaka mitatu na ushei ya kushuhudia mambo yaliyoanza kama vioja yakageuka maudhi kwa wengi.

Ajabu akidi ni kwamba, hata baadhi ya watu waliodhani Trump angalibadilisha Amerika kwa manufaa yao wanalia kwa jicho moja wakifunga jingine kwa kuwa yanayoendelea kushuhudia siyo mabadiliko waliyotarajia.

Juzi nimepita eneo ambapo wakati wa kampeni za uchaguzi uliomweka Trump madarakani, shabiki wake mkuu akipeperusha bendera ya Amerika na kusifia makeke ya kiongozi huyo.

Kilichonishangaza ni kwamba ghafla bendera imeondolewa, maandishi ya kumsifia Trump na kuwakashifu wasiompenda yameondolewa, nafasi ile pakajengwa kitu kinachokaa kama sehemu ya kuwanyongea watu!

Nilijisemesha na kujiambia natumai kwamba shabiki wa Trump hajaathiriwa vibaya na uongozi wa shujaa wake, labda kwa kufutwa kazi au kwa mfumko mkubwa wa bei za bidhaa za kawaida ambao unawaathiri Waamerika.

Ni rahisi kusema kuwa chaguzi zina athari zake, eti hivyo ndivyo mambo huishia tunaposhindwa kutumia akili kufanya maamuzi ya kisiasa.

Tunaweza hata kuwalaumu wafuasi wa Trump waliomweka madarakani, lakini nadhani tunapaswa kutafakari zaidi kuhusu muundo mpya wa siasa duniani.

Ukweli ni kwamba, japo Trump amewaumiza wengi, bado ana mashabiki wengi wanaomchukulia kama zawadi ya binadamu kutoka kwa Mungu, ambaye amekuja kwa ajili ya kusuluhisha matatizo ya muda mrefu.

Mtizamo huo unashikiliwa na wengi duniani, si Amerika tu, ambako wanasiasa wahafidhina na wabaguzi wa rangi wanaonekana kama mashujaa.

Vijana wanaanza kujinasibisha na itikadi kali na katili kama zilizokuwa za nduli wa Ujerumani, Adolf Hitler, aliyewaua Wayahudi 6,000,000 na kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia.

Mshirika mkuu wa Trump na tajiri nambari moja duniani, Elon Musk, ndiye anayeongoza mabadiliko mapya ya kuirarua serikali ya Amerika na kupunguza wigo wake nje na ndani ya nchi.

Musk, mzaliwa wa Afrika Kusini aliyehamia Amerika na kutumia fursa zilizopo kujitajirisha, alilaumiwa sana kwa kupiga suluti ya Hitler wakati wa hafla ya kumwapisha Trump.

Ushawishi wa Musk kwa Trump umesababisha kufungwa kwa mashirika makubwa ya serikali kama vile kituo cha redio cha Sauti ya Amerika (VOA), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Amerika (USAID), kushinikizwa kwa wafanyakazi wa serikali wajiuzulu na kadhalika.

Si hayo tu! Hivi majuzi Musk amemsadikisha Rais Trump kumfukuza balozi wa Afrika Kusini, Ibrahim Rasuul, kwa kile kilichosemekana kuwa ‘kutompenda Trump’.

Hivi tulifikaje huko kwa watu, acha wanadiplomasia, kulazimishwa kumpenda kiongozi wa Amerika? Si hii ni nchi inayoheshimu uhuru wa watu kufunguka na kusema yaliyo nyoyoni zao?

Inaaminika sababu kuu ya Balozi Rasuul kufukuzwa ni sheria dhidi ya makaburu wa Afrika Kusini ambayo ilipitishwa bungeni na kutiwa saini na Rais Cyril Ramaphoosa.

Sheria hiyo inaipa serikali ya Afrika Kusini mamlaka ya kutwaa na kurejeshea wenyewe, aghalabu bila fidia, mashamba ambayo Weusi wa nchi hiyo walinyang’anywa na Wazungu enzi ya utawala wa kibaguzi.

Kwa kuwa tangu hapo nyani haoni kundule, Trump alitangaza hivi majuzi kwamba Amerika imesimamisha misaada ya kifedha kwa Afrika Kusini kutokana na sheria hiyo, akailaumu serikali ya taifa hilo kwa kuendeleza sera za kibaguzi dhidi ya Wazungu.

Kwa mkumbo uo huo, Trump alitangaza kuwa atawapa hifadhi, na hata uraia kwa kasi kuu, Wazungu wa Afrika Kusini ambao watahamia Amerika kutokana na sera dhalimu za serikali yao.

Kumbuka huyo ni yule-yule Trump ambaye anawafukuza wahamiaji wengi Amerika, hasa watu weusi. Ni yule-yule Trump anayependekeza raia wa jumla ya mataifa 22 ya Afrika wawekewe vikwazo vya uhamiaji au wazuiwe kabisa kuingia Amerika.

Unapoisoma makala hii, yapata wafanyakazi 1,300 wa VOA wako nyumbani wakisubiri kujua hatima yao, ama watarejeshwa kazini au watapigwa kalamu.

Kosa lao? Wengi ni wahamiaji, na Trump anashuku hawampendi.

Utakuwa mtu wa aina gani ukalazimisha mgomba kumea changaraweni? Wasikilizaji wa watangazaji hao, angaa 4,000,000 kote duniani, hawapokei matangazo waliyozoea kwa miaka mingi, kisa na maana Trump hapendwi!

Inasemekana kuwa demokrasia hufia gizani.

Huenda wengi waliojifunza haki zao kupitia matangazo ya VOA na kujinasua kutoka kwenye uzingire wa madikteta wakakata tamaa na kusalimu amri, waendelee kukandamizwa.

Fununu zinazoenea ni kwamba Trump na Musk wananuia kuondoa ukomo wa mihula ya urais, Trump awe rais wa maisha.

Ungeniambia hivi mwaka mmoja uliopita ningekucheka, lakini nimejifunza mambo ni kangaja huenda yakaja. Hakuna kinachotabirika. Naam, hata nchini Amerika, nchi iliyojulikana kwa utulivu.

Ni muhimu watu – hasa viongozi wa mataifa yanayoendelea – waelewe kwamba Amerika imebadilika, wajifunge vibwebwe kukuza nchi zao bila kutegemea msaada wa ‘Bwana Mkubwa’.

[email protected]