Tumewasajili wapiga kura 20,754 pekee kufikia Oktoba 8, 2025-Ethekon
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeelezea hofu kwamba huenda ikafeli kusajiliwa idadi lengwa ya wapiga kura wapya 6.3 milioni ikiwa imesajili Wakenya 20,754 kufikia Oktoba 8, 2025.
Kulingana na mwenyekiti wa tume hiyo Erustus Edung Ethekon, kaunti za Nairobi, Mombasa na Kiambu pekee ndizo zimeandikisha zaidi ya wapiga kura wapya 1,000 ndani ya muda wa siku 10 tangu kuanza kwa zoezi hilo Septemba 29, 2025.
Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa kusajili wapiga kuwa wapya 4,804, ikifuatwa na Mombasa iliyoandikisha wapiga kura 1,3 79 huku Kiambu ikiwa imeandikisha wapiga kura wapya 1,203. Kaunti zingine 44 zimesajili wapiga kura wapya wasiozidi 1,000 huku Nyamira ikiwa ndio imesajili idadi ndogo zaidi ya wapiga kura 18 pekee kufikia Oktoba 8,2025.
“Huku tukiwashukuru waliojitokeza kujisajili kuwa wapiga kura kwa mara ya kwanza, japo idadi ya vijana wanaojitokeza ingali ndogo kinyume na tulivyotarajia. Huku tukilenga kusajili wapiga kura wapya 6.3 milioni, IEBC inahimiza Wakenya wote waliohitimu, haswa vijana, kujisajili ili wawe na usemi katika uchaguzi mkuu wa 2027,” Bw Ethekon akaeleza.
IEBC inaendesha shughuli ya usajiliwa wapiga kura wapya katika afisi zake zilizoko katika maeneo bunge, isipokuwa katika maeneo wakilishi 24 ambako chaguzi ndogo zitafanyika Novemba 27, 2025.
Aidha, IEBC imetoa nafasi kwa wapiga kura wanaotaka kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura kufanya hivyo huku wengine wakiruhusiwa kukagua maelezo yao kwenye sajili ya wapiga kura.
Mnamo Septemba `18, Bw Ethekon aliwaambia wabunge kwamba tume hiyo inalenga kuwa na jumla ya wapiga kura milioni 29 kwenye sajili ya wapiga kura kufikia 2027.
“Endapo tutafaulu kuwajili wapiga kura wapya milioni 6.3 ifikapo 2027, sajili mpya ya wapiga kura itakuwa na zaidi ya wapiga 29 milioni ikizingatiwa kuwa kufikia 2022 idadi hiyo ilikuwa na wapiga kura 22.5 milioni,” akaeleza alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC).
Lakini baadhi ya vijana wameripotiwa katika vyombo vya habari wakilalamikia umbali wa afisi za IEBC kama kikwazo cha wao kujitokeza kujisajili.
Wanalalamikia ukosefu wa pesa za kulipa nauli ili wasafiri hadi katika vituo hivyo.
“Baadhi ya maeneo yetu ni mbali na afisi ziko mbali. Kwa mfano, nataka kujisajili katika eneo bunge la Kisauni, Mombasa, lakini wakati huu niko eneo la Jilore, Malindi. Nahitaji Sh600 ili nisafiri hadi Kisauni, pesa ambazo sina,” Baraka Ngumbao, 21, akaripotiwa akisema.
Wengine wanawalaumu maafisa wa IEBC na wanasiasa, kwa kutoendesha kampeni ya kutoa uhamasisho kuhusu shughuli hiyo.