Makala

Uchafuzi wa mazingira Githurai

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MARUFUKU ya matumizi ya mifuko ya plastiki yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2017 yalipokelewa kwa hisia tofauti, baadhi ya walioathirika wakiomba kuongezewa muda.

Hata hivyo, serikali ilishikilia muda hautaongezwa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira, ikisema marufuku hayo yalilenga kuhifadhi mazingira.

Walioathirika pakubwa – hasa wafanyabiashara – hawakuwa na budi ila kukumbatia mifuko inayoruhusiwa.

Waliokaidi amri hiyo walijipata kuandamwa na mkono wa sheria, baadhi yao wakikamatwa na hata kufunguliwa mashtaka.

Juni 2019, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa mwaka 2020 serikali pia itapiga marufuku matumizi ya chupa za plastiki hasa za matumizi ya mara moja tu. Alitangaza hayo akiwa nchini Canada.

Kiongozi wa taifa alisema mikakati ya serikali inaenda sambamba na malengo muungano wa UN kuhifadhi mazingira, UNEP.

Licha ya juhudi za serikali, baadhi ya mitaa Nairobi marufuku hiyo inaonekana haijatekelezwa kikamilifu.

Katika mtaa wa Githurai 44 hali si hali tena kwani mifuko ya plastiki imetapakaa.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebainisha katika mojawapo ya eneo limekuwa jaa la mifuko hiyo.

“Sehemu hii imekuwa ikitupwa kila aina ya uchafu, mifuko ya plastiki ikiongoza,” akasema mmoja wa mkazi aliyeomba jina lake lisichapishwe.

Ni miaka miwili sasa tangu marufuku ianze kutekelezwa, na kulingana na mkazi huyo serikali inapaswa kuweka mikakati kabambe kuona mianya ya kiini cha mifuko hiyo imezibwa kikamilifu.

“Taswira tunayoshuhudia hapa ni wazi mifuko hii inaendelea kuundwa. Inatengenezewa wapi huko serikali haijui?” akahoji.

Baadhi ya bidhaa hutoka kiwandani kama zimepakiwa katika mifuko hiyo. Mkazi mwingine alilalamikia suala hilo akidai marufuku ya 2017 yalilenga mfanyabiashara mdogo.

“Viwanda vinavyounda na kupakia bidhaa zao katika mifuko hiyo pia vipokezwe mjeledi ili lengo la kuhifadhi mazingira liafikiwe ipasavyo,” akasema.

Eneo lililoonekana kuathirika pakubwa li mita chache kutoka kituo cha chifu wa Githurai 44, ambaye pia ana maafisa wa askari tawala, AP.

La kushangaza kandokando mwa eneo hilo kuna kidimbwi ambacho pia kimetiwa mifuko ya karatasi za plastiki na uchafu.

Ni hatari kwa wapita njia na hata watoto kwani kimejaa maji hasa msimu huu wa mvua.

“Si salama kwetu, watoto wamekuwa wakiangukia humu jambo ambalo linatutia wasiwasi sisi kama wazazi,” akalalamika mama mmoja.

Uchafuzi wa aina hiyo mbali na kuhatarisha maisha ya binadamu, unaziba mitaro ya majitaka ambayo ikikosa kutathminiwa maji machafu yatatapakaa na kusababisha Kipindupindu.

Serikali ya kaunti kwa ushirikiano na Nema inapaswa kuangazia suala hili na mitaa mingine ambayo hali yake ni sawa na mtaa wa Githurai 44. Hali ya mtaa huo si tofauti na Zimmerman, Kahawa West na mtaa wa Githurai 45 ulioko Kiambu.