UCHAMBUZI WA VITABU TAHINIWA VYA FASIHI: Maudhui katika Tamthilia ya 'Kigogo'
Na WANDERI KAMAU
Nafasi ya mwanamke
BAADHI ya wahusika wanawake katika tamthilia hii wamesawiriwa kuwa wazalendo na mashujaa, huku wengine wakiibukia kuwa wasaliti na adui za wao kwa wao.
Sera ya uongozi katika jimbo hili pia inaonekana kuwatenga wanawake, ndiyo sababu baadhi yao kama vile Tunu wanaibukia kuwa wapiganiaji ukombozi.
Sudi anapochonga kinyago cha shujaa mwanamke, Kenga anamwambia kuwa Sagamoyo haijawahi kuwa na mwanamke ambaye ni shujaa. Katika historia ya jimbo hilo, wanawake wamekuwa wakitengwa kabisa katika masuala yanayohusu uongozi (uk10).
Kenga anasema kuwa kinyago hicho hakitanunuliwa, ambapo anabadilisha mawazo yake na kusema kuwa afadhali achonge kinyago cha ngao.
Kimsingi, tukio hili linaonyesha dhana hasi iliyo katika nafsi za Wanasagamoyo wengi, kwamba mwanamke hana uwezo wowote, hasa kuhusu masuala ya uongozi.
Wanawake pia wanasawiriwa kuwa washerati (mahawara). Kwa mfano, Sudi anapokataa kuchonga kinyago, Kenga anamwambia kuwa “amelishwa kiapo na hawara wake” (uk12). Hili linaashiria udhalilishaji wa mwanamke na jamii.
Wanawake vilevile wanachukuliwa kama mapambo katika jimbo hilo, kuonyesha kwamba hawana thamani yoyote.
Majoka anamwambia Ashua kuwa urembo wake hauwezi kufananishwa na lolote.
“…nikufananishe na nini? Urembo wako hauna mfanowe Ashua” (uk20).
Majoka anamshauri Ashua atumie urembo wake vizuri kwa kuwa ni wa muda tu (uk25).Wanawake wenyewe wanaonekana kukubali kudhalilishwa kwao, kwani Husda anakubali dhana kuwa wanawake ni kama mapambo tu (uk6).
Wanawake wanasawiriwa kuwa wenye maringo, kwani Majoka anasema Ashua alikataa kazi ya ualimu kutokana na maringo yake (uk 25).
Wanawake wanaibukia kuwa maadui wa wenyewe kwa wenyewe. Kwa mfano, Husda anamwita Ashua kuwa mdaku, kimada wa kuwinda waume wa watu, licha ya nia yake kutokuwa hivyo.
Uongozi mbaya
Jimbo la Sagamoyo linakumbwa na msururu wa migomo na maandamano ya wafanyakazi.
Wauguzi wa Sagamoyo wanaandamana. Walimu wa Sagamoyo pia wanagoma wakiwa likizoni kwa kutolipwa mishahara yao.
Hali hii inaendelea katika jimbo hili kuashiria jinsi uongozi wa Majoka umewatelekeza wafanyakazi kwa kutoshughulikia maslahi yao.
Katika kiwanda cha Majoka and Majoka Company, anakofanya kazi Siti, watu wanagoma kwa kutolipwa mishahara. Vijana watano wanauawa katika harakati za kuitisha mishahara yao.
Hali pia ni tete katika Soko la Chapakazi, ambako wachuuzi wanaandamana wakilalamikia sera mbaya za uongozi wa Sagamoyo na usimamizi wa soko hilo. Baadhi yao wanaumizwa.
Wachuuzi hao wanalalamikia hatua ya uongozi wa Majoka kulifunga soko hilo.
Hali ya maandamano jimboni humo inaonekana kuwa jambo la kila siku, kwani magazeti hayakosi kuwa na picha za watu wakiandamana.
Katika mojawapo ya habari iliyo magazetini, Tunu anaonekana akiongoza maandamano miongoni mwa watu wanaojiita wanaharakati (uk32).Anapowahutubia wanahabari, Tunu anaulaumu uongozi wa Majoka kwa kufuja pesa zilizopaswa kutumiwa kulisafisha soko hilo. Pesa hizo zinafujwa, jambo linalowakasirisha sana wachuuzi. Anasema kuwa uongozi huo unalifunga soko badala ya kulisafisha (uk32).
Licha ya maandamano yanayoendelea, Kenga anamshauri Majoka kuyapuuza (uk34).
Kuna habari kuhusu maandamano kwenye mitandao ya kijamii. Watu wengi wanazidi kuandamana sokoni wakiongozwa na Sudi. Upeo wa maandamano hayo ni pale yanaharibu sherehe za uhuru.
Majoka anatumia polisi kuwatawanya waandamanaji na kuwaumiza wapinzani wake. Tunu anaumizwa mguu. Runinga ya Mzalendo inaingiliwa na uongozi wa Majoka kwa kuangazia masuala ya maandamano katika jimbo la Sagamoyo.
Kutokana na ghadhabu kubwa aliyonayo kwa sababu ya maandamano ya wafanyakazi, Majoka anaamua kufunga vituo vya habari vyote na kubakisha kituo kimoja pekee kinachousifu utawala wake.Anatumia vyombo vya habari kuendeleza nyimbo za kizalendo ili kusifia utawala wake.
Kimsingi, mkakati huu unalenga kuendeleza propaganda kuhusu ufaafu wa uongozi wake. Mojawapo ya propaganda anazoeneza ni kuwa Tunu hawezi kupigania haki za Wasagamoyo kwa kuwa amelemazwa miguu.Majoka hajali kuhusu kifo cha Ngurumo licha ya kuwa mfuasi wake. Badala yake, anaamua azikwe kabla ya jua kutua; hii ikiwa mbinu ambayo hutumiwa na viongozi katika nchi za Kiafrika kuwadhulumu na ‘kuwanyamazisha’ wapinzani wao (uk69).
Watu wengi katika nchi za Kiafrika ambao walizipinga tawala zilizopo wameuawa katika hali tatanishi.Katika tamthilia hii, njama hizi zinadhihirika pale Majoka na Kenga wanapanga njama ya kumweka gerezani Ashua. Hii ni kwa kuwa Ashua anasingiziwa kuzua zogo katika afisi ya serikali.
Kifo cha mhusika Jabali kilipangwa. Hii ni kwa kuwa Jabali alikuwa mpinzani mkuu wa Majoka, na alikuwa na wafuasi wengi sana. Alipangiwa ajali barabarani ambapo baadaye wafuasi wake wanahangaishwa. Tunu anapanga kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha kifo tata cha Jabali. Hata hiyo, Majoka anapopata habari hizo, anapanga kuhusu njia za kumzima. Kuna mifano tele tamthiliani inayodhihirisha maudhui hayo.