Makala

UGANDA: Onyo kwa viongozi dhalimu mapinduzi yaja!

August 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KATIKA historia, mapinduzi ya kiraia yamechangia pakubwa kung’atuliwa ya viongozi wa kiimla wanaokwamilia mamlakani.

Mapinduzi hayo hutokea wakati wananchi wanapochoshwa na udhalimu wa viongozi hao, ambapo huungana kwa kusahau tofauti zao za kikabila, kidini, kisiasa na kitamaduni.

Nchini Kenya, kuungana kwa wananchi kupitia muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2002, ndiko kulipelekea kushindwa kwa utawala wa Kanu.

Rais Mstaafu Daniel Moi, hakuwa na lingine ila kukubali uamuzi wa Wakenya, japo shingo upande.

Vivyo hivyo, mwelekeo huo ndio unaonekana kutokea nchini Uganda, ambapo Rais Yoweri Museveni anakabiliwa na wimbi kali linalotishia kuyumbisha utawala wake wa kiimla.

Wimbi hilo linaloongozwa na mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine nalinaonekana kusambaa kote kote nchini humo.

Hii ni baada ya vikosi vya usalama kumkamata mwanasiasa huyo na wabunge kadhaa wa upinzani, kwa kisingizio cha “kutishia usalama wa kitaifa.”

Hadi sasa, hali ya taharuki ingali tete, huku baadhi ya nchi za kigeni kama Uingereza, zikitoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri Uganda.

Cha kushangaza ni kwamba, Bw Museveni anaonekana kujitia hamnazo kuhusu wimbi hilo, analodai kuwa la “warusha mawe.”

Undani wa maasi dhidi ya Museveni ni kuwa unaongozwa na wabunge vijana, ambao wamechoshwa na utawala wake wa zaidi ya miaka 30.

Kile kiongozi huyu anaonekana kutofahamu ni kuwa mawimbi haya husambaa kama moto wa nyikani, ambapo mwishoni, huwa wanageukwa hata na washirika wao wa karibu.

Mifano dhahiri ya viongozi waliowahi kung’atuliwa mamlakani na mapinduzi ya kiraia ni aliyekuwa rais wa Haiti, Papa Dok, Ferdinard Marcos (Ufilipino), Hosni Mubarak (Misri), Zine Idine Ben Ali (Tunisia), Muammar Gadaffi (Libya) kati ya wengine.

Ingawa baadhi ya mapinduzi hayo yaliendeshwa na nchi za kigeni kama Amerika, ukweli ni kuwa uingiliaji mataifa hayo huwa ni kuwasaidia raia kujikomboa dhidi ya utumwa wa kisiasa.

Uhalisia uliopo ni kuwa katika enzi hii ya mitandao ya kijamii, ni hadaa kubwa kwa kiongozi yeyote kujidanganya kwamba anaweza kuzima mawasiliano ya raia kuhusu mikakati watakayochukua ili kujikomboa.

Mapinduzi hayo ni onyo kwa viongozi wote Afrika kuwa enzi ya udhalimu wa kisiasa zimepitwa na wakati.

[email protected]