MakalaSiasa

Uhuru anavyotumia mawaziri kufufua umaarufu wake nchini

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHARLES WASONGA

KATIKA kipindi cha majuma kadha yaliyopita mawaziri wa serikali wamekuwa wakizuru maeneo mbalimbali nchini wakikagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Wadadisi wanasawiriwa hatua kama mpango wa Rais Uhuru Kenyatta kujijengea umaarufu miongoni mwa wananchi kabla huku muda wake uongozini ukiendelea kuyoyoma.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki jana alisitisha ziara hizo, kwa muda, baada ya wafanyakazi katika wizara mbalimbali za serikali kupatikana na virusi vya corona.

Akitoa amri hiyo Jumatano wiki jana, Rais Kenyatta alisema mawaziri hao watarejelea ziara hizo, za kuhakikisha kuwa agenda za maendeleo za serikali zinafanikishwa katika pembe zote za nchini, baada ya majuma mawili.

Katika mkutano wake na mawaziri, mawaziri wasaidizi na makatibu wa wizara mapema mwezi huu kiongozi wa taifa aliamuru kuzuru miradi mbalimbali ya maendeleo “kutangamana na Wakenya”. Alisema utendakazi wao utatathimiwa, mwezi Septemba mwaka huu, kwa misingi ya kiwango cha ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo chini ya wizara na idara zao.

“Kama njia ya kupima uwajibikaji, Rais alitangaza kuwa ukamilishwaji wa miradi na mipango ya serikali katika pembe zote za nchini ndio kigezo kikuu kitakachotumika kutathmini itendakazi wa mawaziri, mawaziri wasaidizi na makatibu wa wizara,” Msemaji wa Ikulu Kanze Dena alisema kwenye taarifa aliyoitoa baada ya mkutano huo ulioendeshwa kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Hata hivyo, Naibu Rais William Ruto hakuhudhuria mkutano huo, hali inayothibitisha dhana kwamba mpango huo unatekelezwa kuafiki ajenda mahsusi ya Rais Kenyatta zitakazomfaidi atakapostaafu 2022.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo lengo kuu la Rais Kenyatta ni kuacha rekodi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi atakapoondoka mamlakani.

“Bila shaka Rais Kenyatta anataraji kutumia rekodi hiyo kuwashawishi wananchi kuunga mkono mwanasiasa ambaye atampendekeza kuwa mrithi wake kwa imani kuwa kiongozi huyo ataendeleza rekodi hiyo ya maendeleo,” anasema.

“Hizo ziara za mawaziri haswa katika magharibi mwa Kenya na Mlima Kenya ni sehemu tu ya mpango mpana wa Rais Kenyatta kufufua umaarufu wake ambao umefifia kutokana na dhana kwamba amedumaza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake Rais Mstaafu Mwai Kenyatta,” Bw Bigambo anaongeza.

Ndiposa mapema wiki jana mawaziri Peter Munya (Kilimo), John Munyes (Madini), James Macharia (Uchukuzi), Eugene Wamalwa (Ugatuzi), Sicily Kariuki (Maji) na Mutahi Kagwe (Afya) walipiga kambi katika maeneo mbalimbali magharibi mwa Kenya wakikagua miradi kuu ya iliyoanzisha chini ya utawala wa Rais Kenyatta.

Mawaziri hao walizuru kaunti za Bungoma, Kakamega na Trans Nzoia ambapo Bw Macharia alikagua ujenzi wa barabara la Kitale-Suam-Endebbes-Kwanza inaendelea kujengwa.

Naye Kagwe alizuru hospitali ya rufaa ya Trans Nzoia huku Bi Kariuki akizindua mradi wa maji Kiptogot Kolongolo katika kaunti hiyo.

Katika kaunti ya Bungoma Bw Macharia alizindua ujenzi wa barabara ya Misikhu- Brigadier kisha akakagua ujenzi wa barabara ya Kakamega- Navakholo.

Naye Munya alikagua kampuni ya sukari ya Nzoia kisha akafanya mazungumzo na viongozi wa kaunti hiyo kuhusu mpango wa serikali wa kutekeleza mageuzi katika sekta ya sukari nchini kwa ili kufufua sekta hiyo.

Katika kaunti ya Kakamega Bw Munya alikagua kampuni ya sukari ya Mumias, Bw Macharia akakagua barabara kadhaa na uwanja wa ndege wa Kakamega ambao unakarabatiwa kwa gharama ya Sh200 milioni. Naye Bw Munyes alikagua maeneo kadhaa ya uchumbaji madini katika kaunti za Kakamega na Vihiga.

Itakumbukuwa kuwa kabla ya ziara ya mawaziri magharibi mwa Kenya, majuma mawili yaliyopita walizuru maeneo ya Mlima Kenya wakizindua miradi mbalimbali ya serikali kuu.

Bw Munya alizindua mpango chanjoa ya mifugo na kutangaza mageuzi mbalimbali yanayolenga kupiga jeki kilimo cha kahawa na majani chai. Na mwishoni mnamo Julai 4, waziri huyu wa Kilimo alizindua kampeni nyingine ya chanjo ya mifugo katika kaunti mbalimbali za Rift Valley ikiwemo Baringo.

Wakati huo, mwenzake Bw Macharia (Uchukuzi) alikagua ujenzi wa barabara kuu ya Kenol- Sagana- Marua ambayo itagharimu takribana Sh2.3 bilioni. Mradi huo unazinduliwa wakati ambapo wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakiulaumu utawala wa Jubilee kwa kuwatenga licha ya wao kumpigia Rais Kenyatta kura kwa wingi katika chaguzi za 2013 na 2017. Mradi huo utarajiwa kuzinduliwa na kiongozi wa taifa atakapozuru eneo hilo la Mlima Kenya mwezi ujao.

“Mradi wa ujenzi wa barabara kuu ya Kenol-Sagana-Marua ni sehemu ya mpango mpana wa kuunganisha barabara kuu ya Mombasa-Malaba na mshoroba wa Lapsset unaounganisha bandari ya Lamu na mataifa ya Sudan Kusini na Ethiopia kupitia Isiolo. Mradi huo unalenga kuchochea maendeleo ya kufaidi wakazi wa maeneo ya Mlima Kenya, Kaskazini mwa Kenya na hata Pwani,” Bw Macharia alinukuliwa akisema.

Naye Waziri wa Elimu George Magoha amekuwa kiguu na njia akikagua vyuo vya mafunzi ya kifundi (TVET) na vyuo vya mafunzo ya walimu kukagua namna vinavyojiandaa kuafiki masharti ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19 kabla ya kufunguliwa kuanzia Septemba.

Na kabla ya Rais Kenyatta kuzima ziara hizo kwa muda mawaziri Fred Matiang’I (Masuala ya Ndani), Joe Mucheru (ICT), Ukur Yatani (Fedha), Adan Mohammed (Utangamano wa Kikanda) na Kagwe (Afya) walikuwa ameratibiwa kuzuru Isiolo, Marsabit na Moyale kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Robert Shaw ziara ni njia ya serikali ya Rais Kenyatta kuwafumba macho raia baada ya kupambazukiwa na ukweli kwamba haitafanikiwa kutekeleza Agenda Nne Kuu za Maendeleo kabla ya 2022.

“Kimsingi, rais ameng’amua kuwa changamoto kadhaa ikiwemo janga hili la Covid-19 zitahujumu utekelezaji wa nguzo hizo za maendelea katika nyanja ya uzalishaji chakula, ujenzi wa nyumba 500,000 za gharama ya chini, mpango wa afya kwa wote na ustawishaji wa sekta ya utengenezaji bidhaa. Lakini kwa sababu anataka kuathiri siasa za urithi wake, amebuni mbinu mbadala wa kujenga imani ya raia kwa utawala wake,” anasema.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta analenga kusuka muungano wa wanasiasa kutoka Mlima Kenya, Nyanza, Mashariki, Pwani, Rift Valley na Magharibi mwa Kenya ambao miongoni mwao atateua mrithi wake. Katika eneo la Mlima Kenya anaonekana kumnadi aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth huku katika eneo la Magharibi akipania kuwajenga Gavana Wycliffe Oparanya na Waziri Wamalwa.

Katika eneo la Mashariki anatarajia kufanya kazi na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka huku Rift Valley aliwakuza Seneta wa Baringo Gideon Moi na kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto.

Na eneo la Nyanza nyota wake ni kiongozi wa ODM Raila Odinga na Waziri Matiang’I huku Pwani atamtegemea Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho.