Uhuru kuelekea Mlima Kenya kufufua umaarufu ulioyeyuka
Na MWANGI MUIRURI
RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufanya ziara kochokocho katika ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya katika juhudi za kujaribu kuwatuliza wakazi ambao wanahisi hajawafaa kimaendeleo licha ya kuwa madarakani 2013 na 2017.
Pia Rais Kenyatta anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuzima mawimbi ya umaarufu wa Naibu Rais William Ruto miongoni mwa wakazi mashinani.
Wakazi hao wanamwona kiongozi wa nchi kama “msaliti” aliyekosa shukrani kwa mtu aliyemwokoa alipokuwa kwenye meno ya simba, lakini baada ya kunusurika akamgeuka na kushikana na waliokuwa “wakitaka shingo yake”.
Hisia ni kali mashinani miongoni mwa wakazi wa kawaida ambao hawajawahi kuelewa handisheki kati yake na Bw Raila Odinga wa ODM na kiini chake kumgeuka Bw Ruto.
“Ruto ndiye alimsaidia Uhuru kushinda 2013 na 2017. Alitwambia atatawala miaka 10 naye Ruto 10. Mambo yalibadilika wapi akamtupa aliyemsaidia, na kumchukua Raila ambaye alimhangaisha sana? Anafaa ajitokeze wazi atueleze makosa ya Ruto ni yapi? akasema Daniel Kiragu, mkazi wa eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a.
Manung’uniko pia yamesambaa miongoni mwa wakazi hasa wakulima wa kahawa, majani chai, wafugaji ng’ombe wa maziwa na kuku na vijana.
“Alipokuwa akifanya kampeni alikuwa karibu atoe machozi akituomba vijana tusimuache. Alituita ‘jeshi’ akiahidi kutusaidia kupata kazi na kufanya biashara. Baada ya kurudi Ikulu ametugeuka! Biashara zetu zilifungwa, polisi wanatusumbua na hata mikopo hatupati. Amalize muda wake akapumzike. Lakini ametupotezea miaka 10,” kundi la vijana eneo la Roysambu jijini Nairobi likaambia Taifa Leo.
Katika ziara ambazo zinapangiwa Rais maeneo ya Mlima Kenya, kilicho wazi ni kuwa dhamira kuu ni kusambaratisha ushawishi wa Dkt Ruto miongoni mwa wenyeji.
Kwa mujibu wa Naibu wa Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe, Rais atapenya eneo la Mlimani akiwa na ajenda tatu – kuzima ushawishi wa Dkt Ruto, kuwahakikishia wenyeji kuwa kumekuwa na maendeleo chini ya uongozi wake na kuwaraia waunge mkono BBI na mpango wa Rais wa urithi wa Ikulu 2022.
Bw Murathe asema ziara hizo zitasaidia kuzima propaganda za wale wanaosema hakuna cha kujivunia kwa Mlima Kenya chini ya utawala wa Rais Kenyatta.
“Tuko njiani kwenda Mlima Kenya tukiwa na ukweli halisi kuhusu utawala wa Uhuru. Atapindua umaarufu wa Dkt Ruto eneo hilo na wakazi watakuwa wakiimba tu wimbo Uhuru,” asema.
Lakini Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anataja ziara hizo kama zisizo na umuhimu: “Wakazi wangekuwa wamejionea manufaa ya miradi hiyo katika maisha yao. Hawahitaji kuambiwa tumefanya hili ama lile. Kibaki hakuwa akizunguka kusema yale amefanya kwani faida za kazi yake zilisaidia maisha ya wengi hata bila kutangaziwa.”
Suala moja ambalo limechangia umaarufu wa Rais Kenyatta kushuka eneo lake ni wakazi kumlinganisha na Rais Mstaafu Mwai Kibaki katika kupima utendakazi wake.
Mzee Kibaki anasifika sana katika kaunti za Mlima Kenya kwa kufufua miradi ambayo ilikuwa na manufaa ya moja kwa moja katika maisha ya wenyeji hasa katika kilimo, ujenzi wa barabara, stima, mikopo nafuu ya biashara na elimu.
Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Chris Murungaru asema: “Utawala wa Kibaki uliweka msingi wa wananchi wa kawaida kufanya kazi zenye manufaa kwao binafsi kifedha. Hii ilimfanya awe kipenzi cha wengi, vijana kwa wazee. Mafanikio ya Mzee Kibaki yakitumiwa kupima uwezo wa mwingine lazima kuwe na malalamiko makubwa.”
“Ilikuwaje mara baada ya Kibaki kustaafu mikopo nafuu ilitoweka ghafla kwa wananchi wa kawaida, nchi ikaanza kukopa matrilioni, umaskini uliokuwa umeanza kuisha ukarudi kwa kishindo? Mbona Uhuru hangefuata mpangilio wa Mzee Kibaki ambao ulikuwa na manufaa kwa wananchi wa kawaida? Uhuru ni rais wa matajiri tu! Hana muda kwa walalahoi,” Alex Ndung’u, mkazi wa Kieni katika Kaunti ya Nyeri akaeleza.
Rais anatarajiwa kuzuru miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa kuanzia 2014 hadi sasa, njama ikiwa ni kuwaangazia wale ambao wamekuwa wakilalamika kuwa serikali imefanya mengi Mlima Kenya kama waongo.
Lakini wadadisi wanasema haitakuwa kazi rahisi kuwashawishi wakazi kuwa Rais Kenyatta amewafaa katika utawala wake, ikizingatiwa kipindi chake cha utawala kinayoyoma.
Kulingana na Moses Gitari, ambaye ni mwanakamati katika bunge la Mwananchi jijini Nairobi, maelfu ya vijana ambao walikuwa na matarajio mengi katika utawala wa Uhuru wanamwona kama aliyesaliti ndoto zao.
“Akienda kukagua na kuzindua miradi, swali kuu litakuwa kuhusu manufaa ambayo miradi hii imeleta kwa vijana katika kuboresha maisha ya vijana, wakulima na wafanyabiashara,” anaeleza Bw Gitari.
Katibu katika Baraza la Mawaziri, Kennedy Kihara anasema: “Rais atawaonyesha wenyeji kwamba amekuwa na mawazo mema kwao kimaendeleo.”
Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua naye anateta kuwa wandani wa Rais wamejaa unafiki, kwani baada ya kuona umaarufu wake umefifia wameona wamlaumu Dkt Ruto na viongozi wanaomuunga mkono.
“Tuonyeshwe jinsi kutangamana na wananchi tukiwa na Ruto kulitatiza migao ya bajeti kwa miradi hapa Mlima Kenya. Tumekuwa tukisaka nafasi ya kukutana na Rais na serikali yake tumwelezee kuhusu yanayotusumbua lakini tukafungiwa nje.”
Kiranja wa Wengi katika Seneti, Irungu Kang’ata anasema kuwa rais atatoa mwelekeo mpya wa kisiasa eneo hilo na pia kuuza BBI. Anasema kuwa barabara ambazo zimejengwa katika eneo hilo ni nyingi pamoja na miradi ya stima na maji.
Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa, anasema kuwa hakuna shida na Rais kutembelea Mlima Kenya: “Bora aelewe tu kuna hali halisi mashinani. Unaweza ukajaribu kuuza sera lakini kama bado mtu anaumia maishani ni vigumu kubadilisha msimamo wake.”
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro naye anasema: “Hakuna haja ya kubishana na Rais na wandani wake kwa kuwa ikiwa analeta maendeleo, hayo ndiyo tumekuwa tukisukuma tangu 2013.”
Anawashauri wanaompangia ratiba waelewe kuwa kuna yale matarajio ambayo yako na wakulima, wafanyabiashara…wanasiasa, vijana na wakazi wote.