Akili MaliMakala

Ukuaji wa sekta ya chai Barani Afrika  

Na SAMMY WAWERU December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MUUNGANO wa Wafanyabiashara katika Sekta ya Chai Ukanda wa Afrika Mashariki (EATTA) umetangaza kuimarika kwa sekta hiyo Barani Afrika, ukisema hilo linatokana na mikakati thabiti iliyowekwa kuiimarisha.

Kulingana na EATTA, mikakati hiyo ni pamoja na sera za nchi wanachama, ukumbatiaji wa bunifu na teknolojia kufanikisha masoko.

Akizungumza kwenye mkutano wa muungano huo wa mwaka huu, 2025, mwenyekiti wake, Abdi Kadir Hussein alisema sekta ya chai imepiga hatua muhimu licha ya changamoto zinazoendelea kuathiri ushindani wake.

Barani Afrika, sekta hiyo inayoongozwa kwa uzalishaji na Kenya, uuzaji wa chai iliyochakatwa – maarufu kama black tea, Bw Kadir alisema imeandikisha ukuaji mkubwa.

“Hilo linalotokana hasa na mikakati iliyowekwa kufanya kilimo endelevu cha chai, sera za uuzaji na teknolojia bunifu kuongeza thamani,” mwenyekiti huyo wa EATTA alidokeza.

Mkutano wa kufunga mwaka, ulifanyika mnamo Novemba 27 Jijini Nairobi, ukileta pamoja wadauhusika mbalimbali katika sekta ya chai.

Bw Kadir alielezea kwamba sera zilizowekwa na nchi zinazolima chai, Kenya ikiwemo, zimeongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa kiungo hicho cha kunywa huku zikipanua fursa za wakulima kufikia masoko ya kimataifa.

“Chai inasalia kuwa nguzo ya uchumi wetu na kichocheo cha maendeleo ya jamii, ya vijijini na kupunguza umaskini,” alisema.

Sekta ya chai inachangia kiasi kikubwa katika Pato la Taifa (GDP) la Kenya – ikikadiriwa kuwa asilimia 2.

Pia, ni miongoni mwa sekta zinazozalisha mapato makubwa ya kigeni, asilimia 23 hadi 24 ya jumla ya mapato ya fedha za kigeni.

Hata hivyo, licha ya sekta hii kuwa mwajiri wa maelfu ya watu Kenya, bado inakabiliwa na changamoto tele kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi, kuyumba kwa bei za kimataifa na kupanda kwa gharama za uzalishaji zinazokandamiza hasa wakulima wadogo.

Vikwazo vya kisheria na vya udhibiti, pamoja na ushindani mkali kutoka kwa mataifa mengine yanayozalisha chai, Bw Kadir alisema vinaendelea kuhatarisha mafanikio yaliyopatikana miaka ya karibuni.

“Mabadiliko ya ladha na matakwa ya watumiaji hasa kwa chai maalum, pia, yameathiri wazalishaji wa hapo awali. Hata hivyo, hayo pia yamefungua milango mipya ya ukuaji,” alielezea afisa huyo.

Anasema mahitaji yanayoendelea kuongezeka ya chai ya ubora na ya hadhi ya juu, yenye ladha mahususi na chai iliyo tayari kunywa, yanatoa fursa adimu kwa wazalishaji wa Afrika kuongeza thamani na kufikia watumiaji haswa vijana.

Eneo Huru la Biashara Barani Afrika, ndiyo, African Continental Free Trade Area (AfCFTA), Kadir anasema, linatoa fursa kubwa ya kuimarisha biashara ya kilimo ndani ya bara na kupunguza utegemeaji wa masoko ya zamani.

“Ushirikiano, uongezaji thamani na kujikita katika ubora endelevu vitaiimarisha nafasi ya Afrika kwenye soko la kimataifa la chai,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa EATTA, George Omuga, alitaja mafanikio muhimu ya mwaka 2025, yakiwemo kuimarika kwa utulivu wa soko la kunadi chai Mombasa (Mombasa Tea Auction).

Kiwango cha mauzo katika mnada huo kimefikia asilimia 84, kutoka asilimia 51 mwaka uliopita, 2024, huku mnada ukiwa jukwaa la bei ubora.

Shirika la Ustawi wa Majani Chai Nchini (KTDA), tawi la Mashariki mwa Bonde la Ufa, na Rwanda ndizo zimeongoza kwa wastani wa bei ya Dola – $2.98 na $2.92 mtawalia.

“Ingawa kiwango cha chai kilichouzwa kimeshuka kidogo hadi kilo milioni 410 kutoka milioni 445 mwaka 2024, kushuka huko kunahusishwa na uondoaji wa mizigo ya zamani,” Bw Omuga alisema.

Pia, alitaja mafanikio ya utetezi wa sera, yakiwemo kuzuia ada ya usafishaji ya Sh375 kwa mauzo ya nje na kushirikiana na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), kutatua changamoto za ushuru.

EATTA, hali kadhalika, ilifanikiwa kushinikiza serikali kuondoa ushuru kwenye vifaa vya kupakia chai na kupigania kupunguzwa kwa ada za bandari, hatua ambazo Bw Omuga alisema zimepunguza gharama kwa wauzaji nje ya nchi.

Muungano wa Wafanyabiashara wa Chai Afrika Mashariki umefanikiwa kupata wanachama wapya 32 na kushirikisha DTB kama benki mpya kuendeleza biashara ya wanachama, huku ukitatua asilimia 98 ya changamoto za wanachama kwa wakati ufaao.

Ushirikiano wa kikanda, EATTA inasema, uliimarika kupitia mazungumzo na Chama cha Chai Uganda na wadau kutoka Sri Lanka, pamoja na hatua muhimu ya kusaidia kuachiliwa kwa mizigo ya chai iliyokwama Port Sudan.