Makala

Usiku ambao maseneta walimvua mamlaka Gachagua

Na CHARLES WASONGA October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SAA nne na dakika 49 za usiku wa Alhamisi Oktoba 2024, Rigathi Gachagua alivuliwa wadhifa wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya baada maseneta 54 kuunga mkono shtaka la kwanza dhidi yake katika hoja ya kumtimua afisini.

Nao maseneta 13 walipiga kura ya LA kwa shtaka hilo ambapo Bw Gachagua alidaiwa kufananisha serikali na kampuni ya hisa.

Kwa hivyo, kulingana na hoja hiyo, iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, Mbunge huyo wa zamani wa Mathira, alikiuka Vipengele vya 10 (2) (a), (b) and (c); 27 (4), 73 (1) (a) and (2) (b); 75 (1) (c), and 129 (2) ya Katiba.

Pia Bw Gachagua alidaiwa kukiuka kipengele cha 147 (1) cha Katiba  na kipengele cha 131 (2) (c) na (d) cha Katiba hii.

Maseneta pia waliidhinisha shtaka la nne (4) kuhusu kuhujumu Idara ya Mahakama kwa kutisha Jaji wa Mahakama Kuu Esther Maina. Maseneta 51 walipiga kura ya NDIO huku 16 wakipiga kura ya LA.

Kuhusiana na shtaka la tano (5) kuhusu ukiukaji kiapo cha afisi na uaminifu, maseneta 49 walipiga kura ya NDIO huku 16 wakipiga kura ya LA. Maseneta wawili (2) walisusia upigaji kura.

Shtaka la sita (6) kuhusu kutoa matamshi ya chuki na kuchochea ukabila. Maseneta 48 walipiga kura ya NDIO,  maseneta 18 wakipiga kura ya LA huku mmoja akisusia upigaji kura.

Shtaka la tisa (9):  Kwamba Bw Gachagua alihujumu Shirika la Ujasusi Nchini (NIS) kwa kumshambulia Mkurugenzi Mkuu Noordin Haji.

Maseneta 46 walipiga kura ya NDIO, 20 wakipiga kura ya LA huku mmoja akisusia upigaji kura.

Kwa upande mwingine, Seneti ilikataa kuidhinisha mashtaka sita dhidi ya Bw Gachagua yaliyoorodheshwa katika hoja hiyo.

Mashtaka hayo ni kama yafuatayo:

Shtaka la pili (2): Kumhujumu Rais wa Jamhuri ya Kenya kinyume na vipengele vya  147 (1) na 152 (1).

Shtaka la Tatu: Kuwa Bw Gachagua alihujumu na kuingilia utendakazi wa ugatuzi kwa kupinga hatua ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuhamisha wafanyabiashara kutoka Soko la Wakulima hadi soko jipya lililoko kando ya barabara ya Kangundo, eneo bunge la Embakasi Mashariki.

Maseneta 45 walipiga kura ya LA, 19 wakipiga kura ya NDIO huku watatu wakisusia shughuli hiyo.

Shtaka la 6: Kwamba Bw Gachagua alikiuka Sehemu za 13 na 16 za Sheria kuhusu Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kwa kutoa matamshi kuchochea chuki na ukabila.

Maseneta 48 walipiga kura ya LA, 18 wakipiga kura ya NDIO huku mmoja akisusia.

Shtaka la Saba (7): Kwamba Bw Gachagua alikiuka Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi na kushiriki uovu wa utakasaji wa pesa.

Maseneta 53 walipiga kura ya LA, 13 wakapiga kura ya NDIO huku mmoja akisusia upigaji kura.

Shtaka la Nane (8): Kwamba Bw Gachagua alipotosha Umma kwa kutoa kauli zisizo za ukweli na hivyo kukiuka Sheria kuhusu Maadili na Uongozi Bora.

Maseneta 40 walipiga kura ya LA huku 27 wakipiga kura ya NDIO.

Shtaka la 10 (kumi): Kwamba Bw Gachagua alikiuka maadili kwa kumkosea heshima Rais wa Jamhuri ambaye ni kiongozi wa serikali. Maseneta 45 walipiga kura ya LA, 22 hamna aliyesusia shughuli hiyo.

Shtaka la 11 (Kumi na moja): Kwamba Bw Gachagua alikiuka maadili kwa kuwadhulumu maafisa wa serikali hadharani.

Maseneta 47 walipiga kura ya LA, maseneta 18 wakipiga kura ya NDIO huku wawili wakisusia shughuli hiyo.