Makala

Uzalishaji wa mahindi Kenya watinga magunia milioni 75

Na SAMMY WAWERU December 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

UZALISHAJI wa mahindi nchini umeongezeka mara dufu, mwaka huu taifa likitazamia kuvuna zaidi ya magunia milioni 75. 

Waziri wa Kilimo, Dkt Andrew Karanja amesema ongezeko hilo limetokana na hali bora ya anga na mpango wa usambazaji wa mbolea ya bei nafuu.

Mwaka uliopita, 2023, serikali ilizindua programu ya ruzuku ya mbolea ambapo mfuko wa kilo 50 unauzwa Sh2, 500, chini kutoka Sh7, 000.

“Kwa sababu ya hali bora ya anga (akimaanisha mvua) na mikakati ya serikali kusambaza fatalaiza ya bei nafuu, uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka magunia milioni 45 kwa mwaka hadi kati ya milioni 75 hadi 79,” Waziri Karanja akaambia wanahabari kwenye kikao nao Jijini Nairobi.

Kuboreka kwa uzalishaji wa mahindi nchini, Dkt Karanja alisema kumesaidia kupunguza bei ya unga.

Pakiti ya kilo mbili sasa inauzwa kati ya Sh100 hadi Sh180, kutoka Sh200. 

“Unga sasa unapatikana kwa Sh120 na tunatarajia bei hii kushuka zaidi,” Dkt Karanja alisema. 

Alisema serikali itaendelea kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa Sh3, 500 mfuko wa kilo 90, akisema bei hiyo ilipigwa msasa na kuidhinishwa na serikali ili kushusha bei ya unga. 

Kwa sasa, serikali imeweka akiba ya magunia 760, 000 kwenye mabohari ya Bodi ya Kitaifa kuhusu Uzalishaji wa Nafaka (NCPB).

“Serikali inapanga kununua magunia milioni moja zaidi ya mahindi kutoka kwa wakulima, kwa Sh3, 500 kwa kila gunia la kilo 90,” Dkt Karanja akadokeza.

Alisema serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya usambazaji fatalaiza kwa ajili ya msimu wa mvua kubwa 2025.

Alidokeza kufikia Januari, magunia milioni tano ya mbolea yatakuwa yamefika kwenye mabohari ya NCPB kote nchini, na kwamba serikali itashirikiana na maduka ya kuuza bidhaa za pembejeo (agro vets) na vilevile vyama vya ushirika kusambaza mbolea.

Awali, kulikuwa na malalamishi kwamba wakulima wanasafiri masafa marefu kupata pembejeo hiyo, hivyo kugharamika zaidi.

Wakulima waliosajiliwa kidijitali ndio wananufaika kupitia mpango huo.