VALARY AKINYI: Kipaji chake kimevutia NTV na KTN
Na JOHN KIMWERE
‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyolonga na tangia zama zile ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Ni msemo ambao umeonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.
Pia unaonekana unaendelea kudhihirishwa na kina dada wengi tu ambao wameamua kujituma mithili ya mchwa kwenye masuala tofauti katika harakati za kusaka riziki.
Miongoni mwao ni binti, Valary Akinyi anayejivunia kuanzisha brandi ya kuzalisha filamu mapema mwaka huu baada ya kushiriki uigizaji ndani ya miaka saba iliyopita.
”Nimeanzisha brandi iitwayo ‘Bandilisha Arts Production’ ninakolenga kukuza kipaji cha waigizaji wanaokuja wasichana na wavulana,” anasema na kuongeza kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupitia majaribu mengi tu ya maprodyuza wenye kasumba ya kudunisha hadhi ya wasanii wa kike.
Dada huyu anasema amewapa nafasi zaidi ya chipukizi kumi wa kike na wavulana kadhaa ambao ndiyo wameanza kupiga ngoma.
Anadokeza kuwa analenga kukuza talanta za wasanii wanaoibukia maana amejifunza mengi katika muda huo mfupi amekuwa katika sekta ya uigizaji. Hata hivyo anasema analenga kumfikia Lupita Nyong’o anayetesa katika filamu za Hollywood.
Chini ya kundi hilo wamefanikiwa kuzalisha filamu ‘Mambo mambo’ ambayo huenda ikaonyeshwa kupitia K24 TV endapo itakubalika. Muda huu wanashughulikia filamu za TV Series ‘Stucking in the middle’ wanazopania kuziwasilisha Maisha Magic East kabla ya mwisho wa mwezi Julai mwaka huu.
Anasema analenga kuzalisha filamu nzuri angalau kuyapiku makundi mengine hapa nchini ikiwemo Protel Studios na Jiffy Pictures iliyotengeneza filamu kama ‘Maza’ na ‘Moyo’ ambazo huonyeshwa kupitia Maisha Magic East.
Aidha kupitia kundi hilo hutembelea shule za msingi na sekondari kushiriki michezo ya kuigiza kisha kuzungumza na wanafunzi wazo kuwashauri kuhusu masuala tofauti. Kwa jumla huzungumza nao kuhusu madhara ya kutumia madawa ya kulevya pia madhara ya wasichana kupata mimba za mapema wakiwa shuleni.
”Hushauri wasichana wazingatie elimu yao kwanza na wajiepushe dhidi ya mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wenzao pia wanaume wengine,” alisema na kuongeza msichana akipata ujauzito akiwa shuleni huwa rahisi sana kupoteza mwelekeo katika maisha yake.
Anasema hata kama baadaye hupata nafasi kuendelea na elimu wenzake katika rika lake huwa wamepiga hatua kimaendeleo. Kadhalika anasema huwa picha mbaya sana kwa mwanaume kumpa mwanafunzi ujauzito na kumkatizia elimu yake ilhali yeye huwa anaendeleza shughuli zake kama kawaida.
Kadhalika kupitia kundi hilo wamejitwika jukumu la kuzungumza na wanaume kuhusu masuala ya maisha ya siku hizi. Katika mpango mzima wanalenga kusaidia wanaume kupunguza hasira baada ya mizozo ya kifamilia ambazo zimechangia wanawake wengi kupoteza maisha mwaka huu.
Katika uigizaji binti huyu anajivunia kushiriki vipindi tofauti ikiwemo Auntie Boss (NTV), Daktari (KTN), Real Househelps of Kawangware (KTN) na Hullabaloo (Maisha Magic East).