Makala

Vyakula vinavyoweza kuwasaidia wagonjwa wa kisukari

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Parachichi

PARACHICHI linajulikana kwa kuwa na mafuta mazuri kwa ajili ya moyo.

Mafuta ya namna hii kama yanayopatikana kwenye tunda la parachichi yanaweza kuweka sawa usawa wa lehemu mwilini, yanaweza yakapunguza hatari ya mtu kuathirika na magonjwa ya moyo. Hii inamaanisha kwamba ni tunda zuri kwa mtu mwenye kisukari.

Wakati huo huo, parachichi lina nyuzinyuzi na wanga.

Maharagwe

Maharagwe yana nyuzinyuzi za kutosha, lakini pia yana protini bora kabisa kuliko zote isiyo na madhara kama ile ya nyama na hizi ndizo sababu chakula hiki huwa ni kizuri sana kwa mtu mwenye kisukari na mwenye shinikizo la juu la damu.

Vilevile kutumia vyakula vyenye nyuzinyuzi zaidi kunakuondolea hatari ya kukumbwa na mshtuko wa moyo.

Maharagwe yana kiasi kidogo cha wanga na kiasi kingi cha protini, magnesium na asidi amino.

Samaki

Samaki ni chakula bora kwa mgonjwa wa kisukari. Samaki wana omega 3 ambayo ni nzuri kwa mtu anayetaka kuepuka lehemu na kisukari kwa ujumla.

Omega 3 pia ni nzuri kwa mtu mwenye presha ya kupanda na hupunguza uwezekano wa kutokea tatizo la kupoteza kumbukumbu.

Kitunguu saumu

Kitunguu saumu ni kiungo kizuri kwa chakula na pia ni dawa nzuri sana kwa magonjwa mbalimbali mwilini ikiwemo kisukari.

Hata hivyo ili kitunguu saumu kiwe kizuri kama tiba ni vizuri kitumike kibichi yaani bila kupikwa katika moto.

Tufaha

Kuna msemo wa kizungu unasema: ‘An apple a day keeps the doctor away’, ukimaanisha kula tunda moja la tufaha kwa siku kunaondoa uhitaji wa daktari; hasa daktari wa matatizo ya moyo.

Kula tufaha moja tu kwa siku kunaweza kupunguza lehemu mbaya. Kuna aina ya viondoa sumu vilivyomo kwenye tufaha ambavyo huwezi kuvipata sehemu nyingine yoyote na ndivyo ambavyo vinalifanya tunda hili kuwa muhimu zaidi kutumika na mtu mwenye kisukari kila siku.

Karoti

Karoti zina kiasi kingi cha vitamini A, viuaji sumu muhimu ‘beta-carotene’.

Vitamini A ni muhimu sana kwa wenye matatizo ya macho, kuzuia kansa na kinga ya mwili.

Kiufupi, karoti ni muhimu kwa mtu anayesumbuliwa na kisukari.