Wabunge wa ODM roho mkononi uchaguzi ukiwadia
VIONGOZI wa chama cha ODM waliochaguliwa na wale wanaotazamia kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wanajiandaa kwa uchaguzi wa chama katika maeneobunge na wadi, ambao matokeo yake yanaweza kuathiri udhibiti wa chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga, kimetangaza kuwa uchaguzi wa ngazi ya wadi na maeneobunge utafanyika Aprili 7 na 9 mtawalia, baada ya uchaguzi wa mashinani katika vituo vya kupigia kura mnamo Novemba 2024.
Uchaguzi katika maeneobunge unatarajiwa kuwa mapambano makali zaidi ndani ya chama, kwani utawavutia wabunge wanaohudumu na wale wanaotaka kuwania nyadhifa hizo 2027.
Baadhi ya wabunge wa sasa wanahudumu kama wenyeviti wa maeneo yao ya ubunge, na kuna uwezekano mkubwa wao kujitosa tena kutetea nyadhifa hizo au kusimamisha washirika wao kuhakikisha wanadhibiti chama katika maeneo yao.
Aidha, baadhi ya wabunge pia ni wenyeviti wa matawi ya kaunti, kama vile Mbunge wa Makadara George Aladwa (Nairobi), ambao watahitaji kuhakikisha watu wanaochaguliwa katika ngazi ya ubunge ni wale wanaowaunga mkono ili kusaidia kudumisha nyadhifa zao katika ngazi ya kaunti.
Kwa wale wanaotazamia kuwania nyadhifa za kisiasa 2027, kuwa afisa wa chama maarufu eneo fulani kunachukuliwa kama faida kubwa katika kuhakikisha wanapata tikiti ya chama.
Uchaguzi huu ni sehemu ya mpango mkuu wa Bw Odinga wa kuimarisha chama kuelekea uchaguzi wa 2027.
Ingawa ODM huenda ikaungana na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto katika uchaguzi ujao, bado inataka kudumisha ushawishi katika ngome zake za jadi kama vile Nyanza, Magharibi na Pwani.
ODM inalenga kuchagua jumla ya maafisa 77 katika ngazi ya kaunti ndogo na matawi chini ya kamati nne: Kamati Kuu, Wanawake, Vijana, na Wanaoishi na Ulemavu.
Katika Kamati Kuu, wajumbe watachagua Mwenyekiti, Naibu Mwenyekiti, Katibu, Naibu Katibu, Mweka Hazina, Naibu Mweka Hazina, Katibu wa Uratibu na Naibu Katibu wa Uratibu.
Nafasi zingine ni Katibu wa Wanawake, Katibu wa Vijana, Katibu wa Walemavu, Mwakilishi wa Makundi Maalum na maafisa wanane wa ziada watakaohudumu kama Wajumbe wa Kamati.
Chama kilitangaza kuwa uchaguzi utafanyika kwa njia ya makubaliano au kwa kupiga kura kwa kuinua mikono.
Aidha, ODM ilisisitiza kuwa ni wajumbe walioteuliwa katika kituo cha kupigia kura pekee ndio watakaostahili kushiriki kama wapigakura au wagombeaji.