Wafanyakazi walivyoongezeka kutoka 145 hadi 683 katika ofisi ya Gachagua tangu 2022
IDADI ya wafanyakazi katika ofisi ya naibu rais aliyebanduliwa mamlakani, Rigathi Gachagua, iliongezeka kutoka 145 hadi 683 ndani ya miaka miwili.
Haya yalifanyika licha ya Bw Gachagua na Rais William Ruto kudai kuwa, serikali ya Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta haikuacha pesa zozote katika mikoba ya Hazina ya Kitaifa.
Stakabadhi kutoka kwa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) zinaonyesha kuwa, Bw Gachagua alipochukua usukani, alipata wafanyikazi 145 ambao walijumuisha mafundi na wafanyikazi wa nyumba.
Hii ni kwa sababu, baadhi ya wafanyikazi waliondoka baada ya Dkt Ruto kuwa rais.
Kwa mfano, waliokuwa washauri wa Dkt Ruto akiwa naibu rais Anthony Kibagendi na Bw John Chikati, walifanikiwa kuchaguliwa wabunge wa Kitutu Chache Kusini na Tongaren mtawalia katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.
Bw Kibagendi alikuwa mshauri wa masuala ya vijana na Bw Chikati mshauri wa masuala ya Elimu ya Ufundi (TVET) kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa.
Bw Geoffrey Kaituko pia aliondoka na kuwa Katibu wa Masuala ya Bahari.
Idara za Mabadiliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula zilizokuwa chini ya naibu rais, afisi hizo wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, zilihamishwa hadi Ikulu na Rais Ruto kupitia Amri ya Rais.
Stakabadhi za PSC zinaonyesha kuwa, baada ya Gachagua kuingia ofisini, idadi ya wafanyakazi katika afisi yake iliongezeka hadi 627 na Aprili 4, 2023, ikaongezeka hadi 683.
Nyadhifa mpya 56 za ziada ziliundwa kufuatia kuidhinishwa kwa ombi kutoka kwa Bw Patrick Mwangi, Katibu Msimamizi katika Afisi ya Naibu Rais.
“Hii ni kukuarifu kuwa, nyadhifa za ziada katika Ofisi ya Naibu Rais itaongezeka hadi 683,” barua ya PSC kwa Bw Mwangi iliyotiwa saini na Dkt Simon Rotich, aliyekuwa Katibu na Afisa Mkuu Mtendaji wa PSC wakati huo ilisema.
Katika ongezeko hilo kubwa la idadi ya wafanyikazi, Bw Gachagua alipata vitengo vitatu vipya vya washauri kuhusu elimu, uchumi, biashara na uwekezaji.
Mnamo Oktoba 19, 2024, Bw Mwangi aliandika barua ya kutuma wafanyakazi 108 wa afisi ya naibu rais kwa likizo ya lazima.
Lakini Taifa Jumapili ilipompigia simu kuhusu hatima ya wafanyikazi 575 waliosalia, Bw Mwangi alibaini; ‘likizo hiyo iliathiri walio katika nyadhifa za juu pekee.’
Hata hivyo, mnamo Oktoba 23, 2024, wafanyakazi wote wa Bw Gachagua walizuiliwa kuingia katika ofisi zao katika jengo la Harambee Annex ambalo ni ofisi ya naibu huyo wa rais aliyefurushwa.
Alipoulizwa iwapo hali hiyo ingali inadumishwa, alisema; ‘Ilitatuliwa. Timu zilizosalia zinafanya kazi kama kawaida.” Naibu Rais aliyetimuliwa alipewa watumishi wakuu 39 wa ziada ikilinganishwa na 11 waliokuwa chini ya mtangulizi wake na ofisi ya mkewe ilipewa wafanyakazi 87.
Miongoni mwa wafanyakazi wa ngazi za juu walioongezwa walijumuisha msanifu mkuu wa mijengo, mhandisi mkuu, mhandisi mkuu wa stima, mwashi na mpakaji rangi.
Alikuwa pia na kitengo kamili cha huduma za kisheria.
‘PSC imeshauri kwamba, Ofisi ya Naibu Rais itafute Huduma za Ukaguzi wa Ndani kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ambayo hutoa huduma hizo kuu kwa utumishi wote wa umma,’ Dkt Rotich alisema katika barua.
Ilipoidhinisha kuongezwa kwa wafanyikazi katika ofisi ya naibu rais, PSC ilikataa ombi la kumpandisha cheo naibu mkuu wa wafanyikazi wa afisi ya mke wa naibu rais.
Akiwa naibu rais, Bw Gachagua alikuwa na wasaidizi 13 ikilinganishwa na sita waliohudumu chini ya Rais Ruto alipokuwa Naibu Naibu Rais.