Makala

Wahudumu wa matatu walivyovuna hela kama njugu msimu huu wa Krismasi

Na SAMMY WAWERU December 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMA ilivyo ada na desturi nchini, msimu wa Krismasi unapobisha hodi Wakenya wengi hasa wanaoishi mijini husafiri mashambani. 

Aghalabu, husafiri ili kujiunga na jamaa zao wanaoishi mashambani.

Sawa na miaka ya awali, 2024 haikuwa tofauti vituo vya matatu vikijaa abiria.

Idadi kubwa ikiwa inayosafiri kutoka Nairobi kuelekea mashambani, jukwaa la Krismasi wahudumu wa matatu wamelitumia kuvuna hela kama njugu.

Abiria wakifurika kwenye steni ili kujumuika na wenzao Sikukuu ya Desemba 25, ndiyo kilele cha shamrashamra za maadhimisho ya Krismasi, nauli imepanda mara dufu. 

Wahudumu wa matatu wamevuna hela kama njugu msimu huu wa Krismasi 2024, kwa kuongeza nauli mara dufu. PICHA|SAMMY WAWERU

Licha ya siku hii maalum ulimwenguni kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristu, wahudumu wa matatu hawakusaza waliosafiri. 

Kwa mfano, nauli ya Nairobi kuelekea Bungoma abiria walitozwa zaidi ya Sh3, 000.

“Kwa kawaida, hulipa nauli isiyopita Sh1, 500,” akasema Benson Wamalwa mkazi wa Nairobi, japo anatoka Kaunti ya Bungoma.

Akiwa alisafiri na mwanawe anayeishi Nairobi, Bw Wamalwa kwenye mahojiano na Taifa Dijitali alilalamikia kukohoa zaidi ya Sh6, 000.

Hiyo ni safari ya kuenda mashambani pekee, hajafanya mahesabu ya kurejea.

Hata hivyo, alisema ni desturi yake kila msimu wa Krismasi kushirikiana na familia yake pana.

Kuelekea Eldoret, taswira ilkuwa ni ile ile.

“Nyumbani tulipatwa na jambo la dharura, na pamoja na wanafamilia wengine hatukuwa na budi ila kusafiri. Ilishangaza kuenda Eldoret pekee walikuwa wanalipisha Sh2, 000,” akasema Nelly Cheptepgeny.

Wanaotoka Mlima Kenya, mjeledi ulikuwa huohuo

Kuelekea Nyeri, wenyeji wa ngoma hiyo ya naibu rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua, hawakuwa na jingine ila kulipa Sh1, 000.

Nauli kuelekea Kerugoya kutoka Nairobi, nayo pia ilikuwa mara dufu. PICHA|SAMMY WAWERU

Nauli hiyo ilikuwa ya kuelekea Nyeri Mjini, huku Embu ikiwa Sh1, 000 na Meru Sh1, 500. 

Kwa kawaida, Nyeri ada inayotozwa huwa Sh500. 

Nakuru, Jiji jipya lililo karibu kilomita 160 kutoka Jijini Nairobi ambalo huchukua takriban saa tatu na dakika chache kuelekea humo, abiria waliwekelea Sh1, 000. 

“Sababu za nauli kuongezeka ni kuwa gari linapofikisha abiria, kurejea ni vigumu kupata watu,” akasema mmoja wa wahudumu wa matatu za kuelekea Eldoret. 

Kampuni kama vile Super Metro, inayofahamika kutoa huduma zake Jijini Nairobi, ilivuna pakubwa msimu huu wa Krismasi mabasi yake yakionekana kuelekea Eldoret, Kakamega na hata Bungoma.

Baadhi ya wenye magari ya kibinafsi, kama vile Voxy, walitumia mwanya huo kutoa huduma za usafiri. 

Katika baadhi ya vituo vya matatu Nairobi, kwa sababu ya ongezeko la idadi ya abiria lililosababisha magari kuwa haba abiria waliteta kukesha wakisubiri kupelekwa mashambani.

Misongamano nayo haikukosekana katika barabara ya Nairobi – Nakuru, na pia Nairobi kuelekea Mombasa, baadhi ya sehemu.

Matatu kuelekea Nakuru kutoka Nairobi, ikisubiri abiria. PICHA|SAMMY WAWERU