Wakazi Nairobi waanza kunufaika na mradi wa maji wa Northern Collector
MRADI wa maji uliosubiriwa kwa hamu kutatua ukosefu wa maji jijini hatimaye umeanza kusambaza maji kwa wakazi wa Utawala, Nairobi.
Mpango huo maarufu ‘Northern Water Collector Tunnel’ unaonekana kuwa suluhu kwa matatizo yaliyokumba wakazi hao kwa muda mrefu.
Inatarajiwa angalau lita 140 milioni za maji zitaongezeka katika mfumo wa maji kila siku mradi utakapokamilika.
Rais William Ruto alipigia debe mradi huu alipokuwa katika ziara ya kikazi jijini Nairobi zaidi ya wiki moja iliyopita.
Akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Dkt Ruto alisema mradi huu utaleta afueni katika mitaa ambayo imekumbwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Maji ya Nairobi (NWSC) Arnold Karanja amesema wakazi wanapata maji mara mbili kwa wiki.
Bw Karanja anaeleza kuwa nyumba zaidi zinaunganishwa katika mfumo wa maji na zinaendelea kupokea maji mfululizo.
“Si mitaa yote imeunganishwa kwenye mifereji, lakini tunajikakamua kukamilisha mchakato. Waliounganishwa wanapata maji kwa mara ya kwanza. Wafanyakazi wetu wako mitaani na unaweza kuwasiliana nao wakati wote,” akasema Bw Karanja walipozuru Utawala mwisho wa juma.
Aliambia Taifa Leo kuwa mitaa ya Summit Court, Swan Villa, Olympia Estate, Rubis, na Ridgeway inanufaika.
“Nimeishi hapa kwa miaka 24 na hatujawahi kupata maji kutoka NWSC. Ninafurahi kuwa wakati huu tunapata maji mara mbili kwa wiki,” akasema Walter Kamau, mkazi wa Swan Villa.
Kulingana na Bw Sakaja, Northern Collector utatia kikomo miaka ya ukosefu wa maji Lang’ata, Eastlands, Karen na Utawala ambazo hazikuwa katika mfumo wa maji.
“Uhitaji wa maji jijini ni lita 900 milioni kila siku huku kiwango kilichoko kikiwa lita 525 milioni. Maji ya ziada ya lita 140 milioni yatasaidia kupunguza uhaba,” alisema Bw Sakaja wakati wa ziara ya maendeleo Kaunti ya Nairobi.
Kampuni ya maji Nairobi pia imesema mifereji inayotengenezwa kutoka Karen itawafaa wakazi wa Lang’ata huku mradi ukiwa katika kiwango cha asilimia 80 cha ujenzi.
Hivi majuzi Meneja Mkurugenzi wa NWSC Nahashon Muguna aliambia Bunge la Kaunti ya Nairobi kuwa wizi wa maji ni moja ya changamoto ambazo zinazuia kampuni hiyo kuwapa maji wakazi wa Lang’ata.
Handaki la maji ya kilomita 12 ya Northern Collector hutoa maji Murang’a na hupeleka katika Bwawa la Ndakaini – umetengewa fedha kima cha Sh8 bilioni.