Wakenya wachemkia serikali kufuatia ufichuzi wa BBC kuhusu maafisa walioua waandamanaji
WAKENYA wametoa hisia kali baada ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kupeperusha makala yaliyoashiria kwamba huenda Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) lilihusika katika mauaji ya kikatili dhidi ya waandamanaji wasio na silaha wakati wa maandamano ya Juni 25 mwaka jana.
Makala hayo kwa kichwa, Blood Parliament (Bunge la Damu), yamezua mjadala mkali na maswali mengi, huku Wakenya wakitaka waliohusika kuwajibishwa.
BBC inadai kuwa wanajeshi wa KDF walifyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakishiriki maandamano ya amani nje ya Bunge la Kenya.
Kulingana na makala hayo, licha ya maagizo kutoka kwa kamati ya bunge kwa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi Kenya (IPOA) kufanya uchunguzi, hakuna ripoti rasmi iliyochapishwa wala mtu yeyote aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji hayo.
Wakenya wengi walielekeza hasira kwa KDF.
“Nilishtuka kwa kweli kujua kuwa KDF, taasisi ambayo tulikuwa tukiiheshimu sana, ilikuwa sehemu ya huu uovu. Fikiria: askari wa Kenya, aliye na silaha na mafunzo ya kulinda maisha, akimuua raia asiye na silaha kutoka umbali wa mita 25. Nani aliwatuma na nani aliwaagiza?” Willis Evans Otieno, aliandika katika X.
Wengi walilalamika kwamba hakuna aliyechukuliwa hatua.
“Karibu mwaka mmoja na hakuna aliyewajibishwa,” aliandika @KenyaUnchained.
@James041 alisema: “Hatuna nchi”.
Alice Bossy, aliandika katika X: “Nimelilia wapendwa wetu. Inasikitisha sana. Mungu afariji familia zao.”
Hata hivyo, si wote wanakubaliana na taarifa hii.
@Mwana_Hara_Kati alisema, “Siamini vyombo vya habari vya Ulaya kwani walimfunga Gaddafi na Saddam. Kila wakati wanatafuta maslahi yao.”
Lakini, idadi kubwa ya Wakenya wanakubali kuwa filamu hiyo ina ushahidi wa wazi wa usaliti wa serikali.
“Nani aliruhusu hili? Nani aliamuru hili?” alihojo @KenMwohe.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa picha na video zilizorekodiwa na waandishi wa habari na waandamanaji wenyewe, BBC ilithibitisha kwamba vifo vya David Chege, Eriksson Mutisya, na Eric Shieni vilitokea baada ya askari wa KDF na polisi kuwapiga risasi waandamanaji waliokuwa wameinua mikono juu na wengine wakishika bendera ya taifa la Kenya, ishara ya maandamano ya amani.
Video moja ilionyesha askari aliyevalia kiraia akitoa agizo la “uaa!” kabla ya ufyatuaji wa risasi kuanza, huku waandamanaji wakianguka chini baada ya kupigwa risasi.
Pia, wakati wa maandamano haya, waandishi wa habari walinasa picha na video za matukio hayo, na kamera za simu za waandamanaji zilionyesha risasi zikifyatuliwa kutoka kwa maafisa wa KDF. Kila mmoja alirekodiwa katika video kutoka sehemu tofauti, na picha zinaonyesha wazi kwamba waandamanaji hao hawakuwa na silaha wala hawakuwa tishio.
Kwa mujibu wa BBC, walichunguza mavazi ya askari huyo wa KDF ambaye alionekana akifyatua risasi.
Baada ya uchunguzi, BBC ilifanikiwa kutambua mavazi ya askari huyu kwa ufanisi. Hata baada ya risasi hizo, aliendelea kusema kwa sauti ya juu kwa wenzake kwamba waandamanaji waendelee kuuawa.
IPOA ilidai kuwa inawajibika kuchunguza vitendo vya polisi, lakini KDF walijibu kwa kusema kuwa IPOA haijawasilisha ombi lolote la uchunguzi kuhusu maafisa wao waliohusika katika tukio hili.
KDF, kulingana na BBC, ilisema kuwa wao ni waaminifu na wanaheshimu sheria “lakini ni wazi kuwa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya maafisa hao wa KDF walioua waandamanaji.”
Mmoja wa waandamanaji kwa jina la Ademba Allans, alieleza BBC jinsi alivyohofia maisha yake.
“Nilijua familia yangu ingeweza kupoteza mtoto wao, lakini pia nilijua siwezi kuwaacha watu wafe wakati naweza kuwasaidia,” alisema.
Alieleza jinsi alivyokuwa akisaidia walioumia kwa kupigwa risasi.
Katika uchunguzi wao BBC walijitahidi kutafuta majina ya maafisa waliohusika na mauaji haya, lakini hata hivyo hawakufanikiwa kupata majina kamili.