Makala

Walioangamia Endarasha wazikwa serikali ikikalia uchunguzi


HUKU mazishi ya watoto 21 waliofariki kufuatia moto katika bweni la shule ya Hillside Endarasha, Kaunti ya Nyeri yakianza, maswali yanaulizwa kuhusu kimya kinachotawala uchunguzi kuhusiana na mkasa huo.

Waathiriwa tisa wa mkasa huo wa moto walizikwa Alhamisi huku wengine 12 wakizikwa tarehe tofauti zijazo. Wavulana wawili bado wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha kutokana na tukio hilo.

Naibu Rais Rigathi Gachagua aliongoza familia zilizoathiriwa na waombolezaji katika ibada ya wafu iliyojaa hisia za simanzi katika uwanja wa Mweiga eneo bunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Cha ajabu ni kwamba wazungumzaji katika ibada hiyo hawakudai haki kwa waathiriwa 21 wa mkasa huo.

Huku vumbi likitulia kwenye makaburi yao madogo, wasiwasi umetanda kuhusu kile kilichotokea usiku wa Septemba 5 2024.

Hakuna mtu, hadi sasa, aliyekamatwa au kuwajibishwa kwa vifo vya wavulana hao 21 waliochomeka katika bweni na maswali sasa ni kuhusu iwapo haki itapatikana.

Katika usiku wa maafa, kulikuwa na wavulana 164 katika bweni hilo ambalo limebomolewa. Uchunguzi wa Taifa Leo ulionyesha kuwa huenda kulikuwa na msongamano wa wanafunzi ndani ya bweni hilo.

Baadhi ya walionusurika walisema kuwa walitatizika kutoroka kutokana na moto huo mkali kwani kulikuwa na madirisha saba tu na milango miwili, wa tatu ukiwa umefungwa upande wa nje.

“Ni kama Wizara ya Elimu inataka nchi kusahau kwamba watoto 21 waliangamia katika moto katika bweni la shule. Lazima mtu  awajibike. Tutazungumza hadi lini kuhusu mwongozo wa usalama ambao hautekelezwi?” aliuliza Omboko Milemba, mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari Kenya (Kuppet).

Miongoni mwa maswali yanayoulizwa ni pamoja na ukaguzi wa mwisho (ikiwa upo) wa Wizara ya Elimu kabla ya mkasa huo na ikiwa shule hiyo ilikuwa imekaguliwa na serikali ya kaunti kwa kuzingatia kanuni za usalama wa moto.

Pia kuna maswali kuhusu kuzingatiwa kwa nyenzo za ujenzi baada ya kugunduliwa kuwa sehemu ya kuta za mabweni zilijengwa kwa mbao.

Kufuatia masaibu hayo, Rais William Ruto aliahidi uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo lakini siku 20 baadaye, hakuna habari kuhusu uchunguzi huo.

“Naagiza mamlaka husika kuchunguza kwa kina tukio hili la kutisha. Wale waliohusika watawajibishwa,” Rais alisema.

Kitengo cha mauaji katika Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inaongoza uchunguzi na ilirejesha shule hiyo kwa wasimamizi wiki iliyopita.

Polisi wa eneo hilo wameshikilia kuwa uchunguzi unafanywa kutoka makao makuu ya DCI na kwa hivyo hawawezi kutoa maelezo yoyote.

Taifa Leo ilijaribu bila kufaulu kupata jibu kutoka kwa mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. Simu yake ilikuwa imezimwa na alikuwa hajajibu jumbe zetu hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii.

“Timu ya wapelelezi inafanya kazi kila saa, ikirekodi taarifa kutoka kwa watu inayohisi wana habari kuhusu mkasa huo, na imepiga hatua kubwa katika uchunguzi huu,” inasema taarifa ya mwisho kuhusu mkasa huo kutoka kwa DCI ya Septemba 11 2024.

“Tuna nia ya kujua kilichosababisha janga hili. DCI inaongoza mchakato huu. Kama wizara, pia tunafanya ukaguzi ili kubaini kama kulikuwa na dosari yoyote kwa upande wa maafisa wetu. Tutawajibisha mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa tukio hili. Pia tumeagiza ukaguzi wa kitaifa wa shule zote za umma na za bweni ili kubaini iwapo zinafuata Mwongozo wa Usalama wa Shule,” alisema Waziri wa Elimu Julius Ogamba.