Wamarakwet waandaa tamasha ya kwanza ya utamaduni
JAMII ya Marakwet inapanga tamasha ya kwanza ya kitamaduni mnamo Ijumaa 8 Novemba 2024 katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi.
Waandalizi wanalenga kunadi utamaduni wao wenye utajiri kwa lengo la kupitisha maarifa kwa kizazi kijacho.
Tamasha ya Marakwet 2024 inayotarajiwa kuendelea hadi Jumamosi alfajiri imevutia wasanii mbalimbali wa muziki kutoka kwa jamii hiyo na watu mashuhuri.
Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari kilichofanyika Jumamosi jijini Nairobi, Mwenyekiti wa Tamasha ya Utamaduni wa Marakwet John Kisang alisema tamasha hiyo itaonyesha historia nzuri ya hali ya maisha ya Wamarakwet, ambayo inadaiwa kuwa haijawahi kurekodiwa.
“Utamaduni wetu tajiri unaangazia mambo mbalimbali kama vile nyimbo za kiasili, maisha ya kiuchumi, vyakula vyetu na hata mila za kijamii,” alisema.
Bw Kisang alifichua zaidi kuwa lengo la hafla hiyo ni kuonyesha ulimwengu jinsi jamii ya Marakwet inaoana na mazingira asilia licha ya mitindo yao ya maisha kuathiriwa na elimu ya Magharibi.
Katika matamshi yake, Mkurugenzi wa tamasha hiyo na Mratibu Christine Cherop, alibainisha kuwa hafla hiyo pia inalenga kukuza umoja miongoni mwa jamii mbalimbali kupitia kubadilishana ujuzi na utamaduni.
“Tumekuwa tukiandaa hafla kama hizi katika nyumba zetu za kiasili, lakini tulichagua kufanya moja huko Nairobi ili kuwaelimisha vijana wetu ambao hawajaweza kuunganishwa kikamilifu na tamaduni zao,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisisitiza tamasha hiyo itavutia ulimwengu kuelewa historia ya jamii ya Marakwet akibainisha itasaidia kuhifadhi utamaduni.
“Tunataka watoto wetu waelewe utamaduni kwa vile wao ni viongozi wa siku za usoni katika jamii na ulimwenguni kwa kwa ujumla,” aliongeza.
Kikie Kendagor, mwanachama wa tamasha na msimamizi wa habari na mawasiliano, alifichua kuwa jamii ya Marakwet inajiendesha kwa kuzingatia mazingira asilia.
Aliongeza: “Hii ni kwa sababu jamii iko kati ya msitu wa Cherangany na Bonde la Kerio.”
Kendagor alifichua kuwa utamaduni huo unatawaliwa na sheria za kitamaduni ambazo zinaongoza jamii.
“Tamaduni zetu zinatuhitaji tuhusiane na wanyamapori na maliasili.Hii inadhihirika tunapowapa watoto wetu majina ya wanyama pori na misimu kama vile jina la Cherop kutaja mwanamke ambalo linamaanisha msimu wa mvua,” Bw Kendagor alisema.
“Wamarakwet walikuwa wakitabiri misimu au mabadiliko ya hali ya hewa ambapo wangetumia ndege wanaohamahama na wanyama watambaao kama vile milio ya vyura kumaanisha kuibuka kwa msimu wa mvua,” aliongeza.
Bw Kendagor alifichua kuwa mavazi ya kitamaduni kwa jamii yao ni ngozi ya mbuzi na shanga za miguu, haswa kwa wanawake kuashiria uzazi.
Kwa upande wa elimu, alisema kuwa Marakwet watatumia methali, vitu vya kale, matukio ya kitamaduni, mavazi ya kitamaduni na hadithi ili kuwapa maarifa vijana.
“Jambo muhimu zaidi ambalo tunataka kupitisha kwa kizazi kijacho ni sheria zetu za kimila kwa kuwa ni ishara ya utambulisho wetu,” alisema Kendagor.
Alitoa wito wa hitaji la kulinda mfumo wa ikolojia wa asili kwani ni jambo muhimu linalohitajika na jamii ya Marakwet kuhifadhi mfumo wao wa maisha.