MakalaPambo

Wanaume wacheni tamaa, sio rahisi kujitetea kwa kosa la unajisi

Na BENSON MATHEKA November 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA sheria ya makosa ya ngono, unajisi unafafanuliwa kuwa kufanya kitendo cha ngono na mtoto.

Kwanza, ni muhimu kuelewa kwamba mtoto ni mtu aliye na umri wa chini ya miaka 18.

Mtoto hawezi kutoa idhini ya kushiriki kitendo cha ngono na kwa hivyo mtu hawezi kujitetea kwa kusema mwathiriwa alikubali washiriki tendo kama hilo.

Adhabu ya unajisi utegemea umri wa mtoto na mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa miaka kumi na moja kwenda chini anahukumiwa kifungo cha maisha jela.

Kwa watoto wa umri wa kati ya miaka 12-15, anayepatikana na hatia ya kunajisi anafungwa jela miaka ishirini (20) au zaidi, na akidhulumu kimapenzi mtoto wa kati ya umri wa miaka 16-18 atafungwa jela miaka kumi na tano (15) au zaidi.

Mahakama haiwezi kuhukumu mtu anayetuhumiwa kwa kutekeleza unajisi bila kumpa nafasi ya kujitetea.

Mtu anayetuhumiwa kwa unajisi anaweza kujitetea kwa kuonyesha kwamba: Mtoto alimfanya aamini kwamba alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 18 wakati wa kitendo hicho; au aliamini kuwa mtoto alikuwa na zaidi ya miaka 18.

Na hii huwa sio rahisi kwa kuwa ni lazima mshtakiwa  aonyeshe mahakama hatua alizochukua ili kujua umri wa mtoto kabla ya kufanya kitendo hicho.

Utetezi wa aina hii hauwezi kumsaidia mshtakiwa iwapo ana uhusiano wa damu na  mwathiriwa kwa kuwa inachukuliwa alijua umri wake kwa kuwa wana uhusiano wa karibu.

Mtoto akituhumiwa kunajisi mtoto mwingine hawezi kuadhibiwa chini ya Sheria ya Makosa ya  ngono, bali chini ya Sheria ya Watoto na akipatikana na hatia, huwa anatumwa kwa taasisi ya watoto na sio jela.

Mtu anaweza kushtakiwa kwa jaribio la unajisi. Hiki ni kitendo cha kujaribu kushirikisha mtoto katika ngono  na adhabu yake ni kifungo cha miaka kumi (10) jela au zaidi.

Mtu anayetuhumiwa kwa jaribio la unajisi anaweza kujitetea kwa njia sawa na mtu ambaye anashtakiwa kwa unajisi.

Ni muhimu kufahamu kuwa unajisi ni pale mtu anaposhiriki kitendo cha ngono na mtu aliye na umri wa chini ya miaka kumi na minane.

Mtu anaweza kukosa kushtakiwa na unajisi au kujaribu kunajisi na ashtakiwe kwa kushirikisha mtoto katika kitendo cha aibu. Hii ina maana ya kugusa mtoto sehemu za siri, matiti au makalio.

Kushiriki kitendo cha aibu na mtoto adhabu yake ni kifungo cha miaka kumi au zaidi.

Kushiriki kitendo cha aibu na mtu mzima adhabu yake nini kifungo cha miaka mitano  jela au zaidi au kutozwa faini ya hadi Sh50,000  au adhabu zote mbili.