WASONGA: Rotich atangaze mikakati ya chakula cha kutosha
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Fedha, Henry Rotich kesho anatarajiwa kufika bungeni kuwafafanulia Wakenya namna ambavyo Serikali itafadhili bajeti ya Sh3.05 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 unaoanza tarehe moja mwezi ujao wa Julai.
Bw Rotich anasoma makadirio ya bajeti ya mwaka huu wakati ambapo uchumi wa nchi unakabiliwa na changamoto si haba. Serikali hii inakabiliwa na mzigo wa madeni wa Sh5.1 trilioni. Hii ina maana kuwa kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya mwaka huu kitatumiwa kulipia madeni, hasa yale ya kigeni.
Licha ya hayo, Wakenya wanatarajia kwamba bajeti ya mwaka huu italeta afueni katika maisha yao ikizingatiwa kuwa wengi wao wanaathirika pakubwa na hali ya kupanda kwa gharama ya maisha.
Kwa hivyo, Bw Rotich anafaa kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ambazo zinaweza kuwafaidi Wakenya wengi, kama vile kilimo.
Pili, Waziri asiongeze ushuru kwa bidhaa na huduma ambazo hutegemewa zaidi na wananchi wenye mapato ya chini. Badala yake Bw Rotich ahakikishe kuwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) inawaandama wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni ambao hukwepa kulipa ushuru.
Operesheni iliyoanzishwa majuzi ya kuwakamata maafisa wa KRA ambao huhongwa na wakwepaji ushuru inafaa kuendelezwa ili kuhakikisha kuwa asasi hii inatimiza kiwango cha ushuru ilichowekewa.
Kamishna Mkuu mpya James Mburu anafaa kuhakikisha kuwa KRA inakusanya takriban Sh2.1 trilioni katika mwaka wa kifedha unaoanza Julai 1 kama ilivyoelezwa katika makadirio ya bajeti yanayosomwa leo.
Lakini inavunja moyo unapochunguza makadirio hayo ya bajeti yaliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti wiki jana, unapogundua serikali haikutenga pesa zozote za kununua chakula cha hifadhi.
Hali hiyo inaibua hofu ya nchi hii kukabiliwa na kero la uhaba wa chakula sawa na hali ilivyokuwa mapema mwaka huu.
Kutotengwa kwa fedha za kununua chakula cha hifadhi kunaenda kinyume cha azma ya serikali ya kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini, jinsi ilivyoelezwa katika Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.
Bw Rotich anafaa kutangaza mikakati ambayo serikali imeweka kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini endapo mavuno ya mwaka huu hayatakuwa mazuri.
Vile vile, imebainika kuwa kiwango cha fedha kilichotengwa kufadhili mpango wa serikali wa usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima pia imepunguzwa hadi Sh2 bilioni, wakati huu ambapo kuna uhaba wa bidhaa hiyo katika masoko ya humu nchini.
Itakumbukwa kuwa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019, Sh4.3 bilioni zilitengewa mpango huo, lakini ununuzi wa mbolea hiyo kutoka ng’ambo ulicheleweshwa. Wakulima walijipata katika hali ngumu ya kununua mbolea ya upanzi kwa bei ya Sh3,500 badala ya Sh1,800 kwa gunia moja la kilo 50 mapema mwaka huu.
Waziri Rotich pia anafaa kuhakikisha fedha za kutosha zinatengewa sekta ndogo ya kilimo cha unyunyiziaji ili kuimarisha uzalishaji wa chakula.