Afya na JamiiMakala

Watafiti: Kushiriki ngono mara kwa mara kunaimarisha afya

Na CECIL ODONGO March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUSHIRIKI mapenzi mara kwa mara huwa na manufaa tele sio tu ya kimwili, bali pia kisaikolojia, wataalamu wamebaini.

Utafiti huu sasa unashaajisha wapenzi au wanandoa wawe wakishiriki ngono mara kwa mara iwapo wanataka kuishi maisha ya furaha.

Matokeo hayo yanapiga jeki tafiti za awali zilizonyesha kuwa kukosa kushiriki mahaba kwa kipindi kirefu kunaibua wasiwasi, msongo wa mawazo na unyogovu.

Mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi pamoja na akili Dkt Sham Singh anaonya dhidi ya kukaidi hisia zinapochipuka na kukanyagia ngono.

“Kukosa kukata kiu ya ngono bila njia mbadala ya kupunguza msongo wa mawazo hufanya mtu kukasirika haraka, kuwa na wasiwasi na kuhangaika mawazo,” aeleza Dkt Singh.

Mtaalamu huyo pia anasema kuwa ni jambo la aibu iwapo mwanamume au mwanamke atafunguka kuwaambia marafiki zake kwamba hajashiriki mapenzi kwa kipindi kirefu.

Ngono inafahamika husaidia kupunguza maradhi ya moyo na kiwewe kupitia homoni za endorphins.

Homoni hizo pia huchangia mwanamume au mwanamke kuwa na usingizi bora.

Dkt Singh anasisitiza kuwa kutoshiriki mapenzi huleta taharuki ambayo hufanya misuli kukaza, jambo ambalo huibua tatizo la kukosa umakinifu au kupoteza hisia kimwili.

“Haikomi hapo. Wasioshiriki ngono huwa na udhaifu mwilini na mara nyingi hukosa hamu ya chakula,” akaongeza.

Isitoshe, utafiti uliochapishwa 2023 kwenye jarida la Sexual Medicine ulibaini kuwa wanawake walio na umri wa kati ya miaka 20 hadi 59 na wanashiriki ngono mara moja kwa wiki au kukosa kabisa, wako katika hatari ya kuaga dunia mapema.

Hii ni kwa sababu ukishiriki ngono kwa uchache au ukose kabisa, kiwango cha protini huongezeka katika mwili wa wanawake na kusababisha misuli kutanuka.

Ni kutanuka huko kunakoharibu viungo vya mwili na kumletea madhara ambayo huishia hata kuwa kifo.