Makala

WATOTO: Mwigizaji mahiri anayetesa kila afikapo jukwaani

April 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PATRICK KILAVUKA

WAKATI mwingine wanadamu hupenda kutumia hekima yao ya kibinadamu kuyakatiza makusudio ya Mola kwa kujiona kana kwamba wanao uwezo.

Lakini Mwenyezi Mungu huwa na mipango tofuati kwani, mtazamo wake kwa kila mja si sawa na ule wa mwingine japo yeye bado ni yule Mungu Muumba!

Ni kama vile alivyotekeleza azimio lake kwake Yesu baada ya kuupenda ulimwengu na kutimiza azma yake katika mpango wake wa ukombozi kupitia njia ya msalaba pasi na uwezo wa mwanadamu kuyazuia mapenzi yake.

Na hivyo basi wakati maigizo yake Yesu msalabani yanapoigizwa, huwa yanaoneysha kusudio la Rabuka.

Mwigizaji chipukizi Chelsea Wanja (kulia),13, mwanafunzi wa daraja la saba Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Ni katika mchezo wa kuigiza Missing Crown, mwigizaji chipukizi Chelsea Wanja anajaribu kuonyesha jinsi kitu cha thamani cha mja kikipotea huwa hasara kwa mhusika kisipopatikana kwani, unaangazia taji ambalo alikuwa amepewa kama rais wa shule lakini likaibwa na mhusika Backan ( Fidel Ngeso pichani) ambaye ni ndugu yake.

Hata hivyo, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na mwalimu mkuu msimamizi, Kimberly Wairimu, likapatikana.

Mchezo huo uliotungwa na mwalimu John Rickens.

Chelsea, 13, ni mtoto wa pili katika jamii ya Peter Wainaina na Bi Eva Mumbi na mwanafunzi wa darasa saba shule ya msingi ya Visa Oshwal, Nairobi.

Mwigizaji chipukizi Chelsea Wanja (kulia), hufanya mazoezi siku za Jumanne, Alhamisi, Jumamosi na hata Jumapili. Picha/ Patrick Kilavuka

Alianza kugiza mwaka 2017 baada ya mwalimu wa michezo ya kuigiza kumuita baada ya kuona akifanya makeke  ya vichekesho na kujaribu kutathmini utajiri wa kipaji chake na kumsajili katika kikundi cha uigizaji shuleni

“Alinipa mistari kadhaa ya mchezo  kukariri na baada ya kuona vile ninavyozitoa ishara za maigizo na kufua dafu kumilisi uhusika, alinipa nafasi ya mhusika mkuu “Valentine”  katika mchezo uljotajwa,” anasema Chelesa ambaye ujasiri bila uwoga unampa uwezo wa kujasirika mbele ya hadhira, ukakamavu na moyo wa kutokata tamaa umemfaa katika fani hii.

Isitoshe, yeye hufanya mazoezi siku za Jumanne, Alhamisi, Jumamosi na hata Jumapili kama wanajiandaa kushiriki katika mashindano au kufanya michezo ya kuigiza shuleni na hali hiyo,  imempa msingi wa kujiongezea maarifa ya kutia fora katika uwanda huu.

Mwigizaji chipukizi Chelsea Wanja (kulia), anawashauri waigizaji wa rika  yake kufuata maagizo na kujitahidi. Picha/ Patrick Kilavuka

Ingawa hivyo, anasema kama mwigizaji changamoto ambayo huibuka wakati mwingine ni kusahau baadhi ya mistari.

Anagependa kuwa daktari mpasuaji siku za usoni na ameyazingatia masomo ya sanyansi, lugha, hisabati na kuwa mbunifu kana silaha yake ya kujihami na maarifa ya kisanyasi ya kutimiza lengo lake.

Uraibu wake ni kuogelea na kutumbuiza wengine kupitia vichekesho vya kufurahisha.

Ushauri? Uigizaji unahitaji tu kufuata maagizo, kuelekezewa na kujifunza.