Makala

Wazazi wanavyopoteza mamilioni kwa walaghai wanaouza karatasi za KCSE

Na DAVID MUCHUNGUH November 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZAZI, wanafunzi na walimu huenda wanapoteza mamilioni ya pesa kwa walaghai wanaodai wana uwezo wa kuuza karatasi za mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE), unaonyesha uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo tangu mitihani hiyo ilipoanza.

Wale wanaolengwa kuwa wateja hushawishiwa na ahadi za kupewa karatasi za mitihani mapema kuliko watahiniwa wengine. Bei ya kila karatasi ni kati ya Sh2,500 hadi Sh18,000 kwa karatasi za masomo yote na majibu.

Walaghai hao wanaonekana kuwa watu walio na ujuzi wa teknolojia ambao hutumia mitandao ya kijamii ambayo inaonekana kuwa halisi. Wale wanaovutiwa hupewa chaguo la kununua karatasi moja au kujiunga na kundi kuu ili kupata karatasi zote za mitihani, pamoja na majibu.

Hata hivyo, uchunguzi wa Taifa Leo umefichua kuwa ni sakata ya kuwalaghai watu wanaotaka kudanganya katika mtihani ili kupata alama nzuri. Mtandao unaopendelewa zaidi ni Telegram kwa sababu ya usalama wake na huficha utambulisho wa mtu anayetumia akaunti mahususi.

Uanachama katika mojawapo ya chaneli zinazotumika sana kwenye Telegram ambazo tumekuwa tukifuatilia, unaofahamika kama KCSE Leakages 2024 ulipanda kutoka washiriki 50,000 Jumatatu hadi 75,000, jambo linaloonyesha wazi shauku ya watu wengi katika kudanganya katika mitihani.

Juzi, wasimamizi wa kikundi hicho walidai kuwa waliuza karatasi ya mtihani wa Kemia 3 kwa watu 3,589 na kukataa malipo ya wengine 76. Kwa bei ya Sh3,500, hii ina maana kuwa walipata Sh12,561,500 kwa siku moja.

Sheria ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (Knec) ya 2012 inakataza ufikiaji haramu wa nyenzo za mitihani. Sehemu yake inasema: “Mtu yeyote ambaye atapata nyenzo za mtihani na kufichua yaliyomo kwa kujua, iwe kwa mdomo au kwa maandishi, kwa watu wasioidhinishwa, awe mtahiniwa au la, atakuwa amekiuka Kifungu cha 27 cha Sheria na adhabu itakuwa kifungo kisichozidi miaka kumi, au faini isiyozidi Sh2 milioni au adhabu zote mbili kwa pamoja.”

Walaghai huweka picha za karatasi za mitihani kwa siku hiyo dakika chache baada ya mtihani kuanza saa 8.00. Picha hizo zina muhuri wa muda ili kuwashawishi wanunuzi kuwa ni karatasi halisi zilizovuja.

Taifa Leo haikuweza kuthibitisha mihuri hiyo. Mwaka huu, KNEC imebinafsisha nyenzo za mitihani kama mbinu ya usalama na hivyo haijachapisha karatasi zozote za ziada.

Kwa hivyo, wanaohusika na sakata hii wanaonekana kuwa walio na uwezo wa kuzipata. Siku ya Jumanne, tuliazimia kununua Karatasi ya mtihani wa Kiswahili 1, ambayo ingefanywa Jumatano kwa kulipa Sh2,500 zilizohitajika, kwa ahadi kwamba karatasi hiyo ingetolewa kufikia saa 4.00 asubuhi Jumatano.

Ili kuficha utambulisho wao, walaghai hao humshauri ‘mteja’ kulipa kupitia msimbo wa USSD *334# badala ya kutumia programu ya pesa kwenye simu ya mkononi.

Waendeshaji wa chaneli hiyo humuomba ‘mteja’ kuchukua picha ya skrini ya malipo na kuituma kuthibitisha amelipa na kisha asubiri kukabidhiwa karatasi ya mtihani kabla ya kuanza.

Tulilipa kwenye akaunti ya Airtel nambari 108290505 ambayo imesajiliwa kwa jina la Benard Kibet.

Pia tulituma picha ya skrini.

“Asante kwa kutuma picha ya skrini. Tafadhali subiri tunapothibitisha malipo,” ulijibu ujumbe wa moja kwa moja.

Saa 02.37 asubuhi, ujumbe ulifika ukisema: “Kiswahili KARATASI 1 inapakiwa …” Hata hivyo, hadi wakati wa kwenda mitamboni jana, hatukuwa tumepata karatasi hiyo. Wakati huo huo Jumanne, pia tulilipa bei iliyopunguzwa ya Sh12,000 ili kupata karatasi zote za mtihani.

Wakati huu, pesa hizo zilitumwa kwa nambari ya Airtel 100257943 iliyosajiliwa kwa jina la Amos Langat. Kama ilivyokuwa katika tukio la awali, hakuna karatasi za mitihani zilizowasilishwa.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA