Wito nchi wanachama wa COMESA washirikiane kukuza biashara
CHAMA cha watengenezaji bidhaa nchini (KAM) kimetoa wito wa ushirikiano wa kikanda kati ya nchi wanachama wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (Comesa).
Haya yanajiri huku kongamano la Comesa likiendelea jijini Nairobi.
Hafla hiyo, yenye maudhui Kuongeza Uwekezaji kidijitali ili kukuza thamani ya kikanda inawaleta pamoja marais, watunga sera, viongozi wa sekta binafsi, na washirika wa maendeleo kuandaa mkondo mpya wa biashara na ushirikiano wa kikanda.
COMESA inasalia kuwa mojawapo ya muungano wa kimkakati zaidi wa kiuchumi Kenya na chanzo muhimu cha malighafi.
Kwa jumla, Afrika inachangia takriban asilimia 42 ya soko la nje la Kenya, huku COMESA ikichangia asilimia 11 na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) asilimia 30, na Afrika nzima asilimia moja.
Licha ya uwezo wake, biashara ya ndani ya kanda ndani ya COMESA inasalia kuwa ya kawaida, ikichukua chini ya asilimia 12 ya jumla ya biashara kati ya nchi 21 wanachama.
Hii inaangazia haja ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuimarisha ushindani, na kupata bidhaa na huduma zaidi kutoka ndani ya bara.
Tukiangalia mbeleni, Tripartite Free Trade Area (TFTA), ambalo linaunganisha COMESA, EAC, na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) linatarajiwa kusaidia kutatua changamoto za uhusiano wa wanachama huku likifungua fursa mpya za ukuaji na ushirikiano.
Akizungumza wakati wa Kongamano hilo, Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki, alitoa wito kwa nchi wanachama wa COMESA kuongoza uvumbuzi na kukumbatia mabadiliko ya kidijitali ili kuendeleza ukuaji jumuishi.
“Mabadiliko ya kidijitali ndio ufunguo wa kuimarisha thamani kwa ukuaji endelevu na shirikishi. Ni muhimu tukubali uboreshaji wa kidijitali kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi ndani ya COMESA. Zana za kidijitali huwezesha ubunifu na ushindani, hujenga mazingira tofauti zaidi ya biashara, kurahisisha mtiririko wa bidhaa na huduma, na kupunguza taratibu za kutolipa ushuru,” alisema Profesa Kindiki.
Naye Chileshe Mpundu Kapwepwe, Katibu Mkuu wa COMESA, alisisitiza juhudi zinazoendelea za muungano huo kutumia teknolojia kuboresha biashara na kuunganisha uchumi.
“Mjadala mwaka huu utazingatia maeneo manne muhimu ikiwemo biashara ya kidijitali na uwekezaji, tija ya kilimo, na maendeleo ya viwanda,”
“COMESA imetengeneza zana dhabiti za kidijitali ambazo zinaleta mapinduzi katika biashara na ushirikiano wa kikanda, kutoka kwa mifumo jumuishi ya usimamizi wa mipaka na matumizi ya kadi za kisasa ambao unaongeza thamani ya ununuzi katika mataifa yote yanayokumbatia teknolojia.”