Wito wazazi wachunge wanao kufuatia hatari za mafuriko
WAZAZI wametakiwa kuwa makini zaidi na kuhakikisha wanawachunga watoto wao wakati huu wa likizo ndefu ili kuepusha ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika, hasa katika maeneo ambayo huwa na hatari ya mafuriko.
Akizungumza jana na Taifa Leo Dijitali, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Makadara, Bw Philiph Koima alionyesha wasiwasi wake kuhusu usalama wa watoto wanaocheza karibu na Mto Ngong, unaopita katika mitaa ya mabanda ya Mukuru-Kingstone, Mukuru-Lunga Lunga, Mukuru-Sinai, na Mukuru-Paradise katika taraya ya Viwandani.
Bw Koima alisema kuwa kwa sasa shule zimefungwa na wazazi wengi wako kazini, jambo linalowafanya watoto wengi kutumia muda wao wakicheza bila usimamizi.
Alionya kuwa michezo hiyo mara nyingi hufanyika karibu na kingo za mito au maeneo yaliyojaa maji, hali ambayo ni hatari hasa msimu huu wa mvua kubwa.
Alisema kuwa Mto Ngong utajaa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo kama vile Kibera, Ngong, na Upper Hill, jambo linaloongeza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko ya ghafla ambayo yanaweza kuwasomba watoto wasiokuwa waangalifu.
“Tunatarajia mvua kubwa zaidi maeneo ya juu, na hii itasababisha maji ya Mto Ngong kuongezeka. Watoto hawapaswi kucheza karibu na kingo za mto, kwa sababu mara nyingi huvutiwa na maji mengi na wanaweza kujaribiwa kuogelea au kucheza humo,” alionya.
Aidha, Bw Koima aliongeza kuwa matukio ya awali yameonyesha kwamba mto unapovunja kingo zake, wakazi wa maeneo ya karibu hukumbwa na mafuriko, uharibifu wa mali na hata vifo.
Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanabaki nyumbani au wanacheza katika maeneo salama yaliyo mbali na mito na mabwawa wakati huu wa mvua.
Vilevile, aliwataka machifu na manaibu wao, wazee wa Nyumba Kumi na mashirika ya kijamii kushirikiana katika kuhamasisha wakazi kuhusu mbinu za kujikinga na mafuriko na pia kusaidia kufuatilia watoto wanaoonekana wakicheza karibu na maeneo hatari.
Alisema kuwa ushirikiano katika jamii ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa familia kipindi hiki cha likizo ndefu.
Onyo hilo la afisa huyo limekuja wakati Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ikitabiri ongezeko la mvua katika jiji la Nairobi na viungani mwake katika wiki zijazo.
Wakazi wanaoishi karibu na mito au maeneo ya tambarare wametakiwa kuhama kwa muda au kuchukua tahadhari zinazofaa ili kuepuka athari ya mafuriko.
Bw. Koima alisisitiza kuwa usalama wa watoto ni jukumu la wote, na akawataka wazazi kuchukua hatua mapema kabla ya maafa kutokea. “Tusisubiri hadi mtu ataripotiwa kufa maji. Kuzuia ni bora kuliko kutibu,” Bw Koima asema.