Maoni

Maoni: Hivi ndivyo Mwalimu Abduba Dida anavyoweza kutoka gerezani Amerika

Na DOUGLAS MUTUA September 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

HUENDA Mwalimu Mohammed Abduba Dida akaongezewa kifungo gerezani katika nchi ya Amerika iwapo matamshi ya familia yake iliyo nchini Kenya yataifikia serikali ya Amerika.

Bw Dida, aliyewania urais wa Kenya mara mbili (2013 na 2017) anatumikia kifungo cha miaka saba gerezani nchini Amerika kutokana na hali ya kutoelewana iliyozuka kati yake na mkewe wa nne, ambaye walifunga nikaha naye mwaka 2019. Wana mtoto mmoja.

Kuna uwezekano mkubwa wa kesi hiyo kumwendea vibaya zaidi Bw Dida kwa sababu familia yake iliyo Kenya imefichua kuwa ana wake watatu. Alimtaliki mmoja.

Kuoa wake wengi, au kuolewa na wanaume wengi, ni kosa la jinai nchini Amerika. Ikijulikana kuwa mtu umelitenda huadhibiwa bila kusita.

Na si lazima aliyelitenda kosa hilo awe Mwamerika. Kila mtu anayeishi huku. Huwezi kuruhusiwa kuishi Amerika ukiwa na wake wengi hata ikiwa wako nje ya nchi hii.

Utawasikia wahamiaji wakiongea kwa matao ya chini jinsi fulani na fulani walivyo na wake wengi nje ya Amerika, eti wakitaka wake hao wawatembelee hudanganya kuwa ni ndugu zao. Ni siri kuu, lau sivyo ikifichuka tu mtu aozee gerezani.

Ikiwa unataka kuelewa jinsi kosa hilo linavyochukuliwa kwa uzito, fahamu fika kwamba kila anayeomba kibali cha kuhamia Amerika hujaza fomu na kula kiapo cha kusema kuwa hataoa mke zaidi ya mmoja au kuolewa na mwanamume zaidi ya mmoja.

Kimsingi, kiapo hicho husema kuwa ukikiuka sheria hiyo unaweza kushtakiwa kwa kosa la kudanganya chini ya kiapo.

Katika kisa cha Bw Dida, huenda akafunguliwa mashtaka mapya kwa makosa mawili: kusema uongo chini ya kiapo, na kuoa wake wengi. Kesi kama hiyo haiwezi kuendelea kwa muda mrefu kabla haijaamuliwa.

Mkewe Mwamerika anahitaji tu kusema kwamba Bw Dida alimhadaa akafunga ndoa naye bila kujua kuwa tayari alikuwa na wake wengine. Amerika itamwona mwanamke huyo kama mwathiriwa wa ubabe-dume, tabia ambayo inachukiwa sana huku.

Huo ni ushahidi wa kutosha kumweka gerezani mwanasiasa huyo kwa muda mrefu. Pia, hata Bw Dida akikanusha mashtaka kuwa ana wake wengine, taarifa ambazo zimetolewa na familia yake iliyo Kenya na kuchapishwa magazetini ni ushahidi tosha dhidi yake.

Inasemekana kwamba Bw Dida alihamia Amerika mnamo mwezi Januari mwaka 2019 ili kuendelea na masomo, kisha akamuoa mwanamke anayejulikana tu kama Mama Leila.

Ni baada ya wao kukosana ambapo mkewe huyo alimshtaki na akapata kibali cha kumzuia Bw Dida kutangamana naye. Hii ina maana kwamba, kwa maana walikuwa wakiishi pamoja, lazima Bw Dida angeondoka kwenye nyumba ile.

Inasemekana kuwa – labda kutokana na kutoelewa mambo yanavyokwenda kwenye nchi ya watu – Bw Dida alirudi nyumbani huko, akaendelea kuhudhuria swala za Kiislamu kwenye msikiti ambao hata Mama Leila huenda, na alimwandikia jumbe fupi za simu eti.

Huo wote ni ukiukaji mbaya mno wa sheria ambao unaweza kumweka mtu yeyote ndani nchini Amerika, awe mhamiaji, mwenyeji, Mweusi au Mzungu.

Unaitwa uhalifu wa kunyemelea mtu, na unachukuliwa kwa uzito sana kwa sababu kuna visa vingi mno ambapo umeishia kwa vifo vya wanaonyemelewa.

Kosa kubwa ambalo watu wengi, hasa Waafrika, hufanya wanapohamia ughaibuni ni kuchukulia kwamba ile mbinu ya kikale ya kusuluhisha mambo kienyeji inaweza kuwafaa wakiwa ndani ya nchi za watu.

Hiyo ndiyo njia rahisi zaidi ya kujipata ukihamahama kutoka gereza moja hadi jingine ili kuta zipakwe rangi, kwa maana umesota humo si haba.

Nashuku kwamba ni mtizamo huo ambao ulimweka Bw Dida mashakani; labda alidhani kwamba kutagusana na Mama Leila msikitini, kumwandikia ujumbe kwa simu au hata kumtembelea, hata baada ya kuzuiwa na mahakama kufanya hivyo, si kosa.

Kosa jingine kubwa mno alilofanya ni kukosa wakili wakati wa kesi yake, labda kwa kuchukulia kuwa mashtaka dhidi yake yalikuwa hafifu, ama angeshinda au aelewane na mkewe kwa urahisi mbele ya mahakama. Angekuwa na wakili tangu mwanzo, labda kesi hiyo ingeisha hata kabla ya kufikishwa mahakamani.

Hii ni Amerika, si Kenya. Mambo hufanyika tofauti kabisa. Ukiwa na wakili, anaelewana kwa urahisi na mwenzake anayemwakilisha aliyekushtaki, pamoja na jaji au hakimu. Kesi yako huwa rahisi.

Ukitokea mahakamani peke yako, hasa ikiwa wewe ndiwe mshtakiwa, unakaa kama mnyama aliyetoka porini asubuhi, asiyejua kitu kamwe, akaja kufanya kesi na watu waliokwenda shule.

Bw Dida amekata rufaa kwa kuwa anaamini hana hatia inayopaswa kumweka gerezani hadi mwezi Machi mwaka 2029, lakini hata hiyo itakuwa bure kabisa ikiwa hatawakilishwa na wakili.

Akimpata wakili, hata akifunguliwa mashtaka mapya yatashughulikiwa kitaalamu akiwa kimya, tena kwa dakika chache mno, kazi yake iwe kutazama tu.

Kilio cha familia yake iliyo nchini Kenya kwamba serikali ya Kenya iingilie kati hakisaidii kitu. Hizo ni fikra za Kikenya, si za Kiamerika, kwamba mtu aliyefungwa gerezani kwa makosa kama hayo anaweza kuachiliwa huru kutokana na mashauri kati ya serikali mbili.

Hiyo ni kesi iliyofanyika chini ya sheria za Jimbo la Illinois, si serikali ya kitaifa, hivyo hata Rais Joe Biden hawezi kuingilia kati kwa sababu Katiba ya Amerika inamkataza kufanya hivyo.

Hata maombi ya familia ya Bw Dida kwamba kesi hiyo ishughulikiwe chini ya sharia za Kiislamu ni bure; Amerika haitambui sharia, inafuata Katiba yake pekee.

Ikiwa familia ya Mwalimu Dida inataka kumsaidia, hebu na iseme machache mno kwa wanahabari, ifurukute na kumtafutia wakili kwa dharura. Vinginevyo, isubiri kuonana naye mwisho wa kifungo.

[email protected]