Maoni

MAONI: Kalonzo akishikilia uzi huo huo bila kubadilika atafanikiwa 2027

Na CHARLES WASONGA July 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KWA muda mrefu sasa, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa akichukuliwa kama mwanasiasa asiyekuwa na msimamo thabiti, hali ambayo imemgharimu kisiasa tangu 2007 alipowania urais kwa mara ya kwanza.

Aidha, alisawiriwa kama mwanasiasa kigeugeu, ambaye leo anasema hivi na kesho anabadilika na kusema mengine tofauti kabisa.

Kwa mfano, baada kutangazwa kwa matokeo tata ya uchaguzi wa urais 2007, Bw Kalonzo, ambaye alikuwa mmoja wa wagombea urais waliompinga Hayati Mwai Kibaki, alijiunga naye na kuteuliwa Makamu wa Rais.

Hatua hiyo ilionekana kama usaliti kwa wagombea wengine wa urais wakati huo, wakiongozwa na Raila Odinga.

Lakini wakati huu, Bw Musyoka amejitokeza kama mwanasiasa mwenye msimamo thabiti, sifa ambayo imewafurahisha Wakenya wengi.

Kwa mfano, Mbunge huyo wa zamani wa Mwingi Kaskazini juzi alikataa kabisa pendekezo la Rais William Ruto kwamba, kufanyike mazungumzo ya kitaifa kujadili masuala yaliyochangia vijana wa Gen Z kuanzisha msururu wa maandamano.

Aidha, Bw Musyoka amekatalia mbali pendekezo la Rais Ruto la kubuni Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) baada ya kuwapiga kalamu mawaziri wake wote isipokuwa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Musalia Mudavadi.

Dkt Ruto amekuwa akikariri kuwa serikali atakayoiunda itashirikisha wawakilishi kutoka vyama kadhaa vya kisiasa na wadau wengine; wazo ambalo Bw Odinga, ambaye ni kiongozi wa Azimio anaonekana kulikumbatia.

Bw Musyoka alichangamsha wengi Jumamosi wiki jana, wakati wa mazishi ya nduguye Gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya, alipomwambia Bw Odinga peupe kwamba katu hatakubali pendekezo hilo la Rais Ruto.

Kiongozi huyu wa Wiper amepigwa jeki na vinara wenzake kama vile Eugene Wamalwa (DAP-K), kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

Bw Musyoka aendelee kushikilia msimamo huo huo kwa sababu haja kuu ya Rais Ruto ni kutumia upinzani kujitakasa baada ya kuendeleza uongozi mbaya ambao sasa umekataliwa na Wakenya.

Shida ambazo zinazonga utawala wa Dkt Ruto wakati huu ni mwiba wa kujidunga. Alikuwa na nafasi nzuri ya kuzuia yale ambayo anayashuhudia wakati huu endapo angezingatia hitaji la Katiba wakati wa kuunda serikali yake.

Badala yake, Rais Ruto kwa ushirikiano na naibu wake Rigathi Gachagua, waliamua kupendelea watu kutoka makabila yao walipowateua mawaziri, makatibu wa wizara na wakuu wa mashirika mbalimbali ya serikali.