Maoni

Maoni: Raila anakejeli Wakenya kwa kukosoa utekaji nyara wa vijana

Na BENSON MATHEKA December 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WITO wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa serikali ikomeshe utekaji nyara wa Wakenya ni kejeli kuu kwa raia wa nchi hii ambao wanafanyiwa ukatili ambao aliunga mkono alipoamua kushirikiana na serikali.

Alipokubali ‘kusaidia serikali kurekebisha makosa yake’, ilhali inaendelea kuwateka nyara vijana na raia wengine wanaoonekana kuikosoa hasa kupitia mitandao ya kijamii, alikuwa amewasaliti.

Alipokubali kushirikiana na serikali ambayo ilikuwa ikiwateka Wakenya na kuwachukulia kuwa wajinga kwa kukanusha kuhusika, Raila alijiingiza katika uovu huo.

Waziri mkuu huyo wa zamani alikubali kuwa sehemu ya utawala huu alipokubali washirika wake kuteuliwa mawaziri.Na kwa hili, hawezi kuepuka lawama.

Ama kwa hakika, amekunukuliwa akijigamna jinsi alivyopenya na kuingia Ikulu wakati aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa akidai ameweka mitego.

Bw Raila alibomoa upinzani dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza unaohujumu Katiba na kupuuza utawala wa sheria kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha wanaotekeleza haki yao ya kulalamika kwa amani.

Bw Raila mwenyewe aliteka shinikizo za vijana waliotaka serikali iwajibike ikiwa ni pamoja na kukomesha utekaji nyara na mauaji ya raia ambao kosa lao ni kutekeleza haki yao ya kujieleza na kutoa maoni.

Bw Raila alipuuza damu ya vijana waliouawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi wakiandamana wakiwa wamebeba bendera na maji.

Ni juzi tu alipokashifu wanaopinga ushirikiano wake na serikali kwa kufumbia macho mazuri ambayo imetekeleza ilhali wengi, wakiwemo wafuasi wake sugu wanalia.

Ukuruba wake na serikali ambayo inatendea raia ukatili unamfanya sehemu ya uovu ambao anajifanya anakosoa. Sio ajabu hata kumkosoa hapa kukawa hatia.