MAONI: Ruto ajitakase kuhusu madai mazito ya ufisadi yaliyotemwa na Gachagua, Muturi
NIMEWAHI kutaja mara sio moja kupitia ukumbi huu kwamba kikwazo kikubwa kwa maendeleo nchini ni ufisadi.
Mwaka 2019, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alidai kuwa serikali ilikuwa ikipoteza zaidi ya Sh2 bilioni kila siku kupitia uovu huo.
Hii ina maana jumla ya Sh720 bilioni zilikuwa zikiporwa kila mwaka chini ya uongozi wake.
Na mnamo Juni 14, mwaka huo huo, aliyekuwa Balozi wa Amerika nchini Kyle McCarter alionya kuwa serikali (ya Jubilee wakati huo) ingefeli kutekeleza Agenda zake Nne za Maendeleo andapo ingefeli kutokomeza ufisadi.
Alikadiria kuwa serikali ilikuwa ikipoteza zaidi ya Sh800 bilioni kila mwaka, sawa na asilimia 30 ya bajeti yake wakati huo.
Nadhani hii ndio sababu Rais wa sasa William Ruto, mnamo 2023 aliwaahidi Wakenya kuwa serikali yake haingewahurumia wafisadi.
Kulingana naye wafisadi wanapasa kuadhibiwa kwa njia tatu; watupwe gerezani, walazimishwe kuhamia nchi zingine au ‘wapelekwe mbinguni’.
Lakini sasa inashangaza kuwasikia wandani wake wa zamani, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mwanasheria Mkuu wa zamani Justin Muturi, wakidai kuwa Rais Ruto mwenyewe ndiye mfisadi zaidi.
Kwenye mahojiano katika kipindi, “Fixing The Nation” katika runinga ya NTV wiki jana Bw Muturi alifichua msururu wa visa kadhaa za ufisadi vilivyomhusisha Rais Ruto moja kwa moja.
Kwa mfano, Bw Muturi ambaye juzi alivuliwa wadhifa wa Waziri wa Utumishi wa Umma alitoa kisa cha Juni 2023 ambapo kiongozi wa taifa alimlazimu kutia saini mkataba kuhusu ruzuku ya Sh129 bilioni kufadhili mpango wa upanzi wa miti bilioni tatu.
Alidai Rais alitaka pesa hizo zielekezwe moja kwa moja kwa Wizara ya Mazingira badala ya Hazina ya Kitaifa, kulingana na Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma.
Naye Bw Gachagua, kwenye mahojiano na runinga moja ya humu nchini Jumatatu, Aprili 7, 2025 alianika zaidi uozo wa ufisadi serikalini huku akimhusisha Rais Ruto moja kwa moja.
Kile kinachoibua maswali ni baada ya Mbw Gachagua na Muturi kutoa madai yanayomhusisha Rais Ruto na ufisadi, Ikulu ya Rais imechelea kutoa taarifa yoyote kukana au kuelezea ukweli kuhusu sakata hizo.
Kwa kukimya kuhusu madai mazito kiasi hicho, yanayomhusisha mshikilizi wa afisi yenye hadhi kubwa nchini, serikali inatoa nafasi kwa baadhi ya Wakenya kuamini kuwa madai hayo yanasheheni ukweli.
Endapo Ikulu ya Rais itapuuza madai mazito kiasi hicho, bila kutoa maelezo yoyote ya kuyakana, kama ambavyo imekuwa kawaida yake, imani ya Wakenya kwa Dkt Ruto na serikali yake itashuka pakubwa.
Aidha, Rais mwenyewe, ambaye wakati wa kampeni aliahidi kupambana vikali na zimwi la ufisadi, anafaa kujitokeza na kutangaza msimamo wake kuhusu madai hayo.
Majibu yake yatasaidia sio tu kuboresha mustakabali wake, bali kurejesha hadhi ya serikali yake machoni pa umma.
Madai ya Mbw Gachagua na Muturi hayafai kupuuzwa kwani wawili hao wamewahi kuhudumu katika serikali kwa zaidi ya miaka miwili.