Maoni

MAONI: Ruto si mwanafunzi mzuri wa nyakati kwa hivyo ODM itahadhari

Na PAUL NABISWA February 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAMBO lisilopingika ni kuwa Rais William Ruto anataka kuongoza Kenya kwa miaka 10, tena kwa dhati ya moyo wake.

Hatua ya kumtaka waziri mkuu wa zamani Raila Odinga kuongoza Tume ya Umoja wa Afrika (AU) ilikuwa juhudi ya kuondoa mpinzani mahiri katika uchaguzi ujao.

Baada ya Raila kupoteza nafasi hiyo mnamo Februari 15, amekuwa na mkutano naye Mombasa kujadili namna ya ODM na UDA kushirikiana hususan katika uchaguzi mkuu ujao.

Ruto anafurahia haya mazingira, lakini je yatampa afueni 2027? Labda. Yapo mambo ambayo ‘mtukufu’ Rais na Raila Odinga wanatakiwa kuyasoma.

Rais Moi alijaribu kwa bidii kuhakikisha kuwa Bw Uhuru Kenyatta amemrithi katika uchaguzi mkuu wa 2002 bila mafanikio.

Alitumia nguvu za dola, akawa na wanasiasa wa ushawishi na ‘mipango’ kama vile Ruto, Jirongo na Nicholas Biwott lakini Mwai Kibaki akashinda. Moi hakutaka kuamini kuwa kulikuwa na mgawanyiko katika KANU yake.

Kuna watu waliopiga kelele kama Isaac Ruto wakafinywa katika uchaguzi wa mchujo wa KANU.

Leo hii katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna amesema ikiwa Raila ataungana na Ruto wote wataanguka.

Wasiopenda kuambiwa ukweli wamemwona Sifuna kama kichaa.

Mtazamo wa Sifuna haufai kupuuzwa kwa vyovyote vile katika Kenya ya sasa ambayo vijana wa Gen-Z walitetemesha nchi mwaka uliopita.

Baadhi ya vijana hao wanaendana na fikra za mapinduzi za Bw Sifuna na washirika wake.

Si Sifuna tu ndani ya ODM ambaye anadhani kuwa ushirika wa UDA na ODM ni zao la maslahi ya watu binafsi. Seneta wa Siaya James Orengo amekosoa ndoa hii mara nyingi.

Anaona umoja huu huenda ukaficha maovu yanayodhaniwa kutekelezwa na serikali kama vile utekaji nyara na uvunjifu mwingine wa sheria.

Kuna dalili za nyufa kubwa katika chama cha ODM. Hili linatakiwa kuwatisha kama ukoma Rais Ruto na msaidizi wake Raila Odinga wanapojipanga katika mbio za kuingia ikulu milango ya 2027 itakapofunguka.

Hata ndani ya UDA kwenyewe kuna watu wanaodhani kuwa hawa wageni wa ODM “wanakuja sana” kama wanavyosema vijana wa siku hizi.

Suala hili la mabadiliko ya kamati za bunge litaumiza watu wa UDA na watakaopata posho kubwa ni ODM. UDA ni malaika watanyamaza.

Hili la kufukuzwa kwa watu katika kamati kwa manufaa ya wengine alifanya Rais Uhuru Kenyatta.

Waziri Kipchumba Murkomen wakati huo akiwa seneta na Susan Kihika walipokonywa nyama katika Seneti sawa na Prof Kithure Kindiki. Machozi yakawalengalenga.

Watu wakawahurumia. Si hao tu, Bw Moses Wetang’ula alipoteza kiti cha Kiongozi wa Wengi akapewa James Orengo. Akiondoka Papa wa Roma akasema uamuzi huo utafungua mifereji ya vilio.

Hili linatakiwa kuwa funzo kwa Rais Ruto na mwanasiasa nguli Raila Amolo Odinga.

Paul Nabiswa ni mhariri, NTV