Maoni

MAONI: ‘Sauti ya Dhiki’ yauliza, je, hivi sasa Kenya twendapi?

Na JACKTONE NYONJE September 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TAFSIRI ya diwani ya Abdilatif Abdalla ya Sauti ya Dhiki ilizinduliwa Alhamisi, juma lililopita katika taasisi ya Goethe Institute jijini Nairobi na kufwatiwa na majadiliano ya ushairi huu katika tamasha za Macondo Literary Festival Jumamosi, katika Kenya National Theatre.

Voice of Agony ndiyo tafsiri aliyoifanya marehemu Ken Walibora na ikahaririwa vizuri na Annmarie Dury wa Chuo Kikuu cha Yale.

Tafsiri hii ni miongoni mwa tafsiri chache maarufu za Kiswahili katika lugha zingine hususan zile za kimagharibi.

Diwani hii imepata umaarufu kama kazi za mwanzoni kabisa zinazohakiki kwa tafakuri na jicho pevu dhana ya uhuru na suala la baada ya ukoloni, Kenya ikitumiwa kama mfano.

Mashairi aliyoyatunga Abdilatif Abdallah akitumika kifungo cha jela katika magereza ya Shimo la Tewa na Kamiti.

Mashairi yaliyosheheni masuto na ukosoaji wa uongozi wa Kenya baada ya uhuru kwa lugha ya mnato inayoibua hisia, fikra, machugachuga na urazini kuhusu mustakabali wa nchi hii kama taifa huru lililojengeka katika misingi ya kidemokrasia.

Mfumo wa kidemokrasia huwapa wananchi usemi mkubwa. Kauli yao sharti isikike na iheshimiwe. Viongozi wana dhima ya uwakilishi tu inayotokana na Mkataba wa Kijamii, chambilecho Jean Jacquez Rousseau.

Wamiliki wa ruhusa ya uwakilishi ni raia kupitia kwa uchaguzi ulio huru na una zingatia haki na usawa. Mfumo wowote wa uongozi unaokwenda kinyume na mkataba huu huwa umekufuru. Umebadilisha majoho na kuvaa yale ya kiimla.

Udikteta huzima kauli, maoni na ukosoaji wa aina yeyote ule. Huviimarisha vyombo vya ujasusi na dhuluma. Wapinzani na wakosoaji wa mfumo hurambazwa na kutiwa mbaroni.

Makala, machapisho na maandishi ya aina yeyote ili huduhushiwa na kutathminiwa kama ni hatari au ni aula kwa mfumo wa uongozi.

Hii ndiyo sehemu ya historia taifa la Kenya lilipitia kabla kufikia mahali lilipo sasa hivi hususani katika awamu ya kwanza na ya pili baada ya uhuru.

Awamu zilizoshuhudia ahadi tumbi nzuri za mapambano dhidi ya ukoloni zikitumbikizwa katika majaa ya taka na ubinafsi, ukabila, ufisadi, ukiritimba, ujeuri na ukiukaji wa haki za kimsingi ukihanikiza na kuminya koo za utaifa, undugu, umoja, utu, usawa na maendeleo.

Masuala haya yalimsukuma Abdilatif Abdallah kuwa mwanaharakati na kujiunga na vuguvugu la KPU, chama cha upinzani katika awamu ya kwanza. Akilenga kuishinikiza serikali kufanya mageuzi katika mfumo wa utawala.

Dhima yake katika KPU ilikuwa kuandika na kueneza habari kupitia majuzuu mbalimbali. Mojwapo ya juzuu hili lilikuwa la Kenya Twendapi?

Juzuu lililompelekea kukamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya uchochezi na uhaini.

Ni wakati huu akitumika kifungo cha jela alipoyatunga mashairi ya Sauti Ya Dhiki. Sauti ya kilio cha haki na mapambano dhidi ya udhalimu.

Safari inayohitaji msimamo na kujitolea.

Safari iliyo na changamoto nyingi zikiwemo mateso, upweke, vishawishi na unyanyapaa. Bado anasema: ‘N’shishiyelo ni lilo siwati hata tapawa kila kinono’