Maoni

Maoni: Utengano wa Ruto na Mlima Kenya hauna dawa

Na DOUGLAS MUTUA October 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KUVULIWA cheo cha Naibu Rais kwa Bw Geoffrey Rigathi Gachagua hakutakuwa mwisho wa sarakasi, uhasama, masimango na uchokozi – kisa na maana siasa – nchini Kenya.

Hakika, hiyo imekuwa lelemama tu, ndio sasa ngoma inaanza kikweli. Utashuhudia mengi ya kukuburudisha, kukusinya, kukupa kisunzi na kichefuchefu, na hata kukutapisha.

Naam, hayo yote yatakupata, hasa ikiwa bado hujakomaa kiasi cha kujua kwamba hakuna cha kudumu isipokuwa mabadiliko, hasa katika muktadha wa siasa za Kenya.

Nakuhakikishia hivi: Mwanzo huu wa Mlima Kenya kuguswa, kwa maana ya kuanzisha harakati za kumtimua mwanasiasa aliye na mamlaka makuu zaidi kutoka eneo hilo kwa sasa, pia ni mwanzo wa siasa za makabiliano.

Ni utengano hasa kati ya Rais William Ruto na Naibu wake huyo, ambao utaendelea na kudumu hata baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Ngoja nikudokezee kitu; pale Mlimani, ngome ya kisiasa ya Bw Gachagua, hapana msamaha wala maridhiano ya kisiasa ambayo hutokea haraka maslahi ya eneo yakiwekwa kwenye mizani.

Amini usiamini, hata leo hii Dkt Ruto na Bw Gachagua wakiridhiana, na kigogo huyo wa Mlimani ajaribu kuwasadikisha wakazi wa janibu hizo kwamba wagombanao ndio wapatanao, Bw Gachagua atakiona cha moto!

Mkondo wa siasa za eneo hilo hutegemea wananchi wa kawaida, si viongozi wao, na tayari kule mashinani Rais Ruto amekuwa kiti-moto Saudia.

Haliki, anachefua na anatapisha tayari. Kukosana kwake na Bw Gachagua hakuishii hapo; wafuasi wa Bw Gachagua watamsaidia kumchukia na kumuambaa Bw Ruto kama jini kuanzia sasa na hata baada ya kustaafu.

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta angaungana na Bw Gachagua kuwarai wenyeji wamkumbatie Dkt Ruto tena, hilo haliwezekani.

Hata Dkt Ruto angamteua mwanasiasa mwingine kutoka Mlimani kuchukua nafasi itakayoachwa wazi na Bw Gachagua, ikiwa hataponea kwenye Bunge la Seneti au Mahakama ya Upeo, hawawezi kumsamehe.

Ni kwa kuogopa adhabu ya wananchi wa eneo hilo ifikapo 2027 ambapo baadhi ya wanasiasa wanaotoka huko walinywea na kughairi nia ya kuunga mkono shughuli ya kumtimua Bw Gachagua.

Walioshupaa shingo wanasubiriwa kwa hamu na ghamu mashinani, na nakuhakikishia kitawaramba vizuri sana. Hivyo ndivyo zilivyo siasa za Mlima Kenya.

Bila shaka Rais Ruto si limbukeni wa siasa, hayo ni mambo aliyo na satua nayo kikweli, na haikosi ana mpango madhubuti wa kuchaguliwa tena na kuhudumu kwa muhula wa pili, salama pasi na kutishiwa, bila uungwaji mkono wa eneo la Mlimani.

Hata hivyo, sharti nimtahadharishe: Asipotafuta njia ya kuzigawanya kura milioni nne na ushei za eneo hilo, atakuwa na kibarua kigumu mno kuchaguliwa tena.

Kwake kupata asilimia 50 ya kura, na angaa kura moja ya ziada itakiwavyo kikatiba, hakutakuwa mteremko. Labda azaliwe na nyota ya jaha katika uchaguzi wa marudio.

Njia pekee ya Rais Ruto kugawanya kura za eneo hilo, japo hii pia itapata vizingiti tele, ni kumteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa Kithure Kindiki, kuchukua nafasi ya Bw Gachagua.

Akifanya hivyo, huenda akawashawishi watu wachache katika maeneo ya Embu, Kirinyaga na Meru kumuunga mkono.

Wakazi wa maeneo hayo, ambayo yako mashariki mwa Mlima Kenya, wamekuwa wakinung’unika kwa uangalifu kwamba wananyanyaswa kisiasa na magharibi mwa Mlima huo, yaani Nyeri, Murang’a, Kiambu na Nyandarua.

Dkt Ruto akiokota kura kadha huko, kisha aungwe mkono na kinara wa Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga, pamoja na Amani National Congress (ANC) ya Bw Musalia Mudavadi na Ford Kenya ya Spika Moses Wetang’ula, atakuwa ameuweza Mlima.

Nimesalitika kufanya hisabati ya kisiasa kwa kuwa chaguzi mbili zilizopita zimenifunza mengi. Tukumbushane: Katika Uchaguzi wa mwaka 2022, Dkt Ruto alimshinda Bw Raila kwa kura 240,000 hivi.

Tofauti kati yao ilikuwa ndogo hivyo, hata baada ya Dkt Ruto kupata karibu milioni nne za Mlima Kenya. Hata ikiwa hujui hesabu, milioni nne ni kubwa kuliko 240,000, au sio?

Amini usiamini – Bw Odinga asingalijikwaa kwa kumteua Bi Martha Karua kuwa mgombea-mwenza katika uchaguzi uliopita na kumpuuza Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper – angalimshinda Dkt Ruto.

Vipi tena? Bw Odinga alipowania urais, naye Bw Musyoka akiwa mgombea-mweza mnamo mwaka 2017, eneo la Ukambani lilimpa jumla ya kura 1.12 milioni. Kura 300,000 ni nyingi kuliko kura 240,000.

Idadi ya kura alizopata Bw Odinga kutoka Ukambani ilikuwa ndogo – 800,000 pekee – mnamo mwaka 2022 kwa sababu Bw Musyoka hakuwa mgombea-mwenzake.

Bi Karua alimuumiza Bw Odinga kisiasa kwa kuwa hakumzolea kura zozote kwenye eneo la Mlima Kenya anakotoka, lakini inaeleweka kuwa Bw Odinga alishinikizwa na Bw Kenyatta kumteua.

Kumbuka bado ni mapema mno kujua iwapo Bw Odinga atawania urais kwa mara ya sita au atamuunga mkono Dkt Ruto.

Hilo la kuwania si la kufikirika tu, linawezekana. Asipochaguliwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) msubiri kwenye debe!

Kwa ufupi, Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa na ushindani mkubwa zaidi kuliko chaguzi nyinginezo ambazo tumewahi kushuhudia nchini Kenya. Hautabiriki.

Sasa jongea nikumegee niliyotoa kwenye shughuli wa kumtimua Bw Gachagua. Niliifuatilia kwa makini kama mwandishi na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, na vile-vile kama ripota wa zamani wa mahakamani.

Nililazimika kutumia tajriba yangu hiyo kwa kuwa najua huenda mchakato huo ukaishia mahakamani, tena Bw Gachagua ameapa habanduki ng’o mpaka aone hatima ya mchakato wenyewe!

Kwa maoni yangu, hakuna ushahidi wa kutosha kumkuta na hatia katika mahakama yoyote. Mengi yalikuwa madai hafifu tu, na alipopewa fursa ya kujitetea, alitoa ithibati kadha za kuyakabili. Hilo likitokea mahakamani… subiri uamuzi wa mwisho.

Lakini kwa sababu uamuzi wa juzi ni wa kisiasa na ulikuwa umefanywa kitambo, hapakuwa na fursa yake kuponea kwa kuwashawishi wabunge kwa ithibati hizo.

Bunge la Seneti na Mahakama huzingatia ithibati na ushahidi, si sarakasi za kisiasa. Mambo yatakuwa tofauti huko.
Kwa kuwa Kenya ni taifa la kisheria, ni heri tusubiri mchakato mzima ukamilike, uamuzi wa mwisho ukitolewa tuukubali, hata ikiwa shingo-upande tu.