Maoni

MAONI: Yashangaza waliochagua Kenya Kwanza ndio wanashambulia Raila kuhusu Adani

Na CECIL ODONGO October 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TABIA ya baadhi ya Wakenya, hasa waliopigia utawala wa Kenya Kwanza kura mnamo 2022, kumlaumu Raila Odinga kwa matatizo ya nchi haifai hata kidogo.

Mnamo Jumapili kulikuwa na ‘moto’ mitandaoni baada ya Bw Odinga kutangaza kuwa anaunga mkono shughuli za kampuni ya Adani Group nchini.

Hii ni miezi michache tu baada ya kukashifiwa kwa kusambaratisha maandamano ya Gen-Z.

Akiwa Mombasa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la ODM, Bw Odinga alisema kukashifu Adani yenye asili na usuli India bila kutathmii sifa ya uwekezaji katika sekta mbalimbali ambazo kampuni hiyo imefanya, hakufai sini.

Kimekuwapo kilio na malalamishi kuhusu mpango wa kukodisha uwanja wa kimataifa wa ndege (JKIA) kwa Adani kwa kipindi cha miaka 30.

Wiki jana, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi alitangaza kuwa Adani imepewa mkataba wa Sh96 bilioni wa kujenga na kuweka nyaya za umeme nchini kwa muda wa miaka 30.

Pia kuna gumzo kali kuhusu kampuni ya Adani kupewa zabuni ya Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHA).

Waziri huyo mkuu alisema afadhali kutia saini kandarasi hiyo na Adani kuliko kutafuta mikopo kutoka mashirika mbalimbali ya kifedha ilhali imeshalemewa na madeni.

Ni utetezi huu ndio umemweka Bw Raila pabaya miongoni mwa Wakenya hasa wakosoaji wa serikali ambao kinaya ni kuwa wengi wao ndio walipigia utawala huu kura mnamo 2022.

Wafuasi wa Kenya Kwanza wanastahili kumeza mate machungu na kuvumilia serikali ‘yao’ badala ya kumkemea Bw Raila kila mara anapofanya maamuzi yanayowiana na mipango tata ya serikali waliyoichagua.

Ndiyo, utawala huu una changamoto zake na umekosa kutimiza malengo ya wapigakura lakini hilo halina maana kuwa Bw Raila ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kuunga maamuzi hayo.

Katika uchaguzi uliopita, wanaolalamika walimwona Bw Odinga kama asiyefaa ndipo wakampigia kura Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua ambao kwa sasa hawaonani ana kwa ana.

Kukitokea shida kuhusu sera za serikali ambazo zinawafinya raia, ni vyema wao wao wazipinge badala ya kumtaka Bw Raila, 78 ajibwage barabarani na kuandaa maandamano.

Bw Raila ni mwanamageuzi aliyepigania mfumo wa vyama vingi nchini, akasaidia kuleta katiba mpya ya 2010 na kuwafaa wanasiasa wakuu nchini mbali na kuwasaidia kupata uongozi lakini wakamsaliti baadaye.

Katika kila uchaguzi amekuwa akikataliwa na baadhi ya Wakenya ambao sasa wanapiga kelele kuwa ‘anakula’ na serikali na kusahau majukumu yake ya upinzani.

Je, kwani Bw Raila pekee ndiye aliyeandikiwa kuwa upinzani? Hata hao wanaolalamika kuhusu Adani, SHA, JKIA na kadhalika, wana haki ya kikatiba kushinikiza serikali itekeleze mabadiliko.

Kama mkongwe, Bw Raila anastahili kutulia kisha kuunga maamuzi anayoyaona kustahili kwa sababu amejaribu kupambania mageuzi bila mafanikio.

Hao wanaomlaumu walimpinga walipoona shughuli zake kama zilizotishia washikilizi wa mamlaka kutoka jamii zao.

Kumlaumu Raila kwa matatizo ya nchi hakufai bali. Sote tuvumilie serikali hii hadi 2027 ili iwe funzo. Hapo ndipo Wakenya watakuwa na fursa ya kuwachagua viongozi wanaofaa.