Mataifa yanayoendelea yatamweza Trump?
TAIFA la Sudan Kusini limepigishwa magoti na Amerika hivi majuzi! Limesalimu, likampisha Mwamerika ili lisivunjwe mbavu bure.
Ukiona cha mwenzio kikinyolewa, chako tia maji. Busara hizo za wahenga zinaweza kutumiwa na mataifa yanayoendelea, hasa wakati huu wa misukosuko mikuu ya uhamiaji na vita vya kiuchumi.
Amerika na Sudan Kusini zilikosana pale Sudan Kusini ilipokataa kumpokea mtu aliyefukuzwa na serikali ya Rais Donald Trump kwa kuwa mhamiaji asiyekuwa na kibali cha kuishi Amerika.
Sudan Kusini ilimkataa mtu aliyeitwa Bw Nimeri Garang alipofika kwenye Uwanja wa Ndege wa Juba kwa kuwa, baada ya kumhoji, ilithibitishwa jina lake halisi ni Bw Makula Kintu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Idara ya Uhamiaji ya Sudan Kusini ilisema Bw Kintu mwenyewe alisema aliondolewa Amerika bila hiari yake, tena akalazimishwa kwenda Juba.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika, Bw Marco Rubio, alichemka kwa hasira na kulipa kisasi mara moja! Alitoa amri iliyowazuia raia wote wa Sudan Kusini kuingia Amerika.
Hili liliishtua Sudan Kusini sana kwa sababu kadha, ila nitajadili mbili kuu: Uhai wa serikali ya taifa hilo, na mapato inayopokea kutoka kwa raia wake wanaoishi nje.
Ni siri iliyo wazi kwamba serikali ya Sudan Kusini inaishi kwa ganga-ganga za mganga aitwaye Amerika. Rais Salva
Kiir anajua fika kwamba asingehurumiwa na kusaidiwa na Amerika, hangedumu mamlakani hata kwa siku mbili.
Anaongoza serikali aliyolazimishwa na Amerika kuiunda, hivyo Waamerika wakitaka kumtimua mamlakani watafanya hivyo kwa wepesi wa kuajabiwa.
Kwa kutambua hilo, kwake yeye ni heri kumpokea raia wa kigeni asiyejulikana kwao ni wapi hasa, akamtafutia kwao na namna ya kufika huko baadaye, badala ya kung’olewa madarakani. Inaeleweka.
Nimekwambia Rais Kiir anaongoza serikali ya kulazimishiwa kwa kuwa yeye na makamu wake, Dkt Riek Machar, ambaye amefunga kifungo cha nyumbani, ni moto na pamba. Hawapatani kwa lolote kwa kuwa Dkt Machar pia anataka kuwa rais.
Kifungo hicho cha nyumbani kisikushtue; labda hata ni pendekezo la Amerika, katika jaribio la kuhakikisha Sudan Kusini kunakalika na kutawalika.
Miaka kadha iliyopita, wakati ambapo Rais Kiir na Dkt Machar walikosana vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka nchini mwao, Dkt Machar, kwa maelekezo ya Amerika, alifungwa kifungo cha nyumbani Afrika Kusini.
Wakati wote ambapo makubaliano ya kuunda serikali ya sasa yalikuwa yakiandikwa, Dkt Machar alikuwa Afrika Kusini akishughulikiwa kama mradi wa Amerika.
Alirejea Sudan Kusini baada ya Rais Kiir kukubali shingo upande kumshirikisha, pamoja na waasi wenzake, kwenye serikali yake. Dkt Machar si muasi wa kawaida kwa kuwa ana wapiganaji wake wengi tu ambao hukabiliana na majeshi ya serikali ikibidi.
Tangu hapo hali ya kutoaminiana imetamalaki kati ya wawili hao, kwa hivyo nakuhakikishia hata msukosuko wa sasa utaishia kwa wao kushinikizwa na Amerika kuunda serikali ya pamoja.
Huenda Rais Kiir, kwa kuhofia kutimuliwa, na nafasi yake kukabidhiwa Dkt Machar, alikubali shuruti za Amerika kuhusu uhamisho wa Bw Kintu.
Kando na kunyong’onyea kwa serikali ya Rais Kiir, sababu nyingine ya kusalimu amri ni kwamba mapato makubwa ya Sudan Kusini yanatoka nje, hivyo yanaweza kuzuiwa.
Taifa hilo linategemea mapato ambayo hutumwa nyumbani na raia wake wanaoishi ughaibuni, hasa mamia ya maelfu ambao wako Amerika.
Rais Trump, mtu na kichaa chake hasa, anaweza kuamka siku moja na kutoa amri inayosema kwamba raia yeyote wa Sudan Kusini anayetuma pesa nyumbani anaingia hatiani.
Amri kama hivyo ikitolewa hata dhidi ya taifa imara kama Kenya, serikali itafanya kila iwezalo ili kuhakikisha uhusiano wa kawaida kati yake na Amerika umerejea.
Mataifa yanayoendelea yatalazimika kutafuta mbinu ya kukataa shuruti za Rais Trump wakati huu ambapo anajaribisha mbinu kadha za kuvuruga utulivu wa dunia kwa maamuzi ya kutia hofu kuu.