Maoni

Raila atapasuka msamba akiwania kupendeza Gen-Z na Ruto kwa wakati mmoja!


KINARA wa Azimio la Umoja Raila Odinga amejipata katika njiapanda kati ya kuunga mkono vuguvugu la vijana, almaarufu Gen-Z na Rais William Ruto kwa wakati mmoja.

Rais Ruto tayari ametangaza kuwa baraza lake la mawaziri litajumuisha Upinzani na litakuwa na ‘sura ya kitaifa’. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Rais Ruto ametengea Upinzani nafasi tano katika baraza la mawaziri, zikiwemo wizara za Fedha na Kawi.

Lakini Bw Odinga amekuwa akijikokota kutoa orodha ya watu anaopendekeza kuwa mawaziri wa wizara hizo tano.

Vinara wenzake wa Azimio akiwemo kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, wameshikilia kuwa hawatajiunga na serikali ya Kenya Kwanza.

Kujitenga kwa vinara wenza wa Azimio kumemwacha Bw Odinga akikuna kichwa huku asijue la kufanya. Mashirika ya kijamii na baadhi ya Gen Z wanamtaka Bw Odinga kuepuka kujiunga na serikali.

Wandani wa Bw Odinga katika chama cha ODM wanamsukuma kukubali ofa ya Ruto ili wanufaike na nyadhifa hizo.

Inaonekana shinikizo hizo zimemweka Bw Odinga katika kona mbaya.

Hivi majuzi Bw Odinga alitoa masharti anayotaka yatimizwe na serikali ya Kenya Kwanza kabla ya kukubali kufanya mazungumzo na Rais Ruto.

Baadhi ya mazungumzo hayo ni kulipwa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa maandamano, kuachilia huru waandamanaji wote, kupunguza gharama ya maisha na kushtakiwa kwa maafisa wa polisi walioua waandamanaji kati ya matakwa mengineyo.

Matakwa hayo yanalenga kufurahisha Gen Z na mashirika ya kijamii. Ikiwa kweli Raila ameahidiwa wizara na Rais Ruto, hana budi kuzichukua mara moja.

Masharti aliyotoa anaweza kuyatekeleza akiwa ndani ya serikali.

Mathalani, ikiwa chama cha ODM kitapewa Wizara ya Fedha, kitatumia fursa hiyo kubuni mikakati ya kupunguza makali ya deni la nchi na kupunguza gharama ya maisha.

‘Mawaziri wa Upinzani’ pia wanaweza kushawishi Rais Ruto kukubali kuchukulia hatua maafisa wanaoua waandamanaji.

Upinzani unaweza kutumia fursa hiyo kupunguza gharama ya umeme iwapo watapewa wizara ya Kawi kama wanavyoripotiwa katika vyombo vya habari.

Lakini hatua ya Bw Odinga kungoja mabadiliko yatekelezwe ndipo wajiunge na serikali ni kupoteza wakati.

Wahenga walisema mtaka yote hukosa yote—vivyo hivyo Bw Odinga atajipata amekosa nafasi za uwaziri alizotengewa na Rais Ruto huku akichukiwa na Gen Z na vinara wenzake wa Azimio.

Bw Odinga akumbuke kwamba mwenda njia mbili hupasuka msamba.

Rais Ruto anaweza kubadili nia na kuunda baraza lake la mawaziri bila kujumuisha Upinzani na kuacha wandani wa Bw Odinga wakidondokwa na mate.