Maoni

MAONI: Rais Ruto asijitie hamnazo, ashughulikie hisia za raia

Na CHARLES WASONGA October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SINA shaka kwamba, Rais William Ruto alifuatilia kwa makini matukio na hisia za Wakenya mnamo Ijumaa na Jumamosi wiki jana katika vikao vya kushirikishwa kwa maoni yao kuhusu hoja ya kumbandua naibu wake Rigathi Gachagua.

Vile vile, ilivyo ada, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) lilimpasha habari kuhusu matukio ya siku hizo mbili na, bila shaka, athari zake kwa utawala wake ndani ya miaka mitatu iliyosalia.

Ukweli ni kwamba, wananchi wengi hawachukulii kwa uzito mchakato huu wa kumwondoa afisini Bw Gachagua.

Wanahisi kuwa hilo silo zoezi ambalo Bunge na Serikali zinapasa kulipa kipaumbele wakati kama huu.

Wananchi waliojitokeza, katika vituo mbalimbali kwa ajili ya kutoa maoni yao kuhusu hoja hiyo, walitaja wazi wazi masuala ambayo wangetaka viongozi hao washughulikie kwanza.

Masuala hayo ni kama vile changamoto zinazokumba mpito hadi Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF), mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu na vyuo vya kadri, sakata ya ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adan, migomo ya kila mara ya wafanyakazi wa sekta muhimu miongoni mwa mengine.

Wananchi wanahisi huu mchakato wa kumng’oa mamlakani Bw Gachagua unalenga kufaidi wanasiasa na viongozi fulani serikalini huku wao wakiendelea kuteseka na changamoto za kila aina.

Nakubaliana kabisa na hisia za Wakenya hawa ambao wanaonekana kuvunjwa moyo na viongozi waliowachagua miaka miwili tu iliyopita.

Sababu ni kwamba, viongozi hawa wanaonekana kuwatumia kuhalalisha ajenda zao za kibinafsi kwa kizingizio cha kutimiza hitaji la kipengele cha 10 cha Katiba la kushirikisha maoni ya umma katika maamuzi yenye umuhimu kitaifa.

Inatarajiwa kuwa, baada ya Bw Gachagua kuondolewa baadhi ya wanasiasa na maafisa wakuu serikalini watafaidi kwa kutunukiwa nyadhifa mbalimbali.

Tayari, majina ya watu fulani ambao ni wandani wa Rais Ruto yameanza kutajwa wakipigiwa upatu kujaza nafasi yake.

Wabunge wanaosukuma ajenda hii pia wanatarajiwa kufaidi kwani Gachagua akiondolewa, wabunge wandani wake watapoteza nafasi zao kwenye kamati mbalimbali katika asasi hiyo ya kutunga sheria.

Hii ndio maana, tofauti na masuala mengine yenye umuhimu kwa raia, ajenda hii ya kumng’oa Bw Gachagua inaendeshwa kwa kasi zaidi.

Hali hii inawakera raia wa kawaida kiasi kwamba, baadhi yao sasa wameibua kauli ya “kufa dereva kufa makanga” yaani, Bw Gachagua aondolewe pamoja na bosi wake, Rais Ruto.