Maoni

TAHARIRI: Mechi kubwa zipewe marefarii wenye uwezo na uzoefu

September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HATUUNGI mkono fujo za mashabiki uwanjani, lakini sharti uchunguzi wa kina ufanywe kubaini kinachosababisha visa hivyo vya uhuni kabla ya hatua mwafaka kuchukuliwa.

Ni siku chache tu tokea adhabu itolewe ya Shabana kucheza mechi tano mfululizo za nyumbani bila mashabiki uwanjani kwa madai ya kusababisha vurugu katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex, wikendi iliyopita.

Shabana ilikuwa ikiongoza mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) kwa 2-1, kabla ya Ulinzi kusawazisha katika muda wa nyongeza.

Ingawa Ijumaa jioni adhabu hiyo iliwekwa kando na Mahakama ya Kutatua mizozo Michezoni (SDT), kulingana na adhabu hiyo, Shabana itagharamia uharibifu uliotokea siku hiyo, matibabu ya waamuzi walioumia pamoja na maafisa waliosimamia mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 2-2.

Ikitoa uamuzi huo, Kamati ya Ligi na Mashindano (LCC) ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) iliamua kufuata ripoti ya Kamishna wa mechi hiyo, bila kumchukulia adhabu yoyote mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo kufuatia madai ya kupuuza sheria huku akipendelea Ulinzi Stars hadharani.

Ni jambo la kusikitisha kuona kamati hiyo inayoongozwa na Michael Majua Ouma ikipuuza kuthibitisha madai hayo ya uonevu.

Visa vya aina hii vimewahi kutokea hapo awali, huku FKF ikichukuwa muda mrefu kutoa uamuzi, lakini Wakenya walishangazwa na adhabu ya haraka dhidi ya Shabana hata kabla ya chanzo cha fuzo hizo kugunduliwa.

Katika juhudi za kuzima janga hili, lazima FKF ishirikiane na walinda usalama kufuatia maoni ya timu zilizoathirika na kuthibitisha madai ya kuonewa.

AFC Leopards, Tusker FC, Shabana na Sofapaka ni miongoni mwa timu zilizodai kuchezeshwa na waamuzi walioingia uwanjani timu pinzani kupata ushindi kwa mkato.

Miongoni mwa suluhisho ni pamoja na kuanzisha mafunzo, kutumia mbinu za kupima ubora wa waamuzi, huku wasiofaa wakianikwa hadharani na wachanganuzi wa masuala ya soka.

Huku kukiwa na madai kwamba baadhi ya waamuzi hawakupata mafunzo ya kutosha, huku wengine wakichezesha mechi kiushabiki, itakuwa bora iwapo mechi kubwa zitapewa waamuzi wenye uwezo na uzoefu.

Utaratibu wa masomo kuboresha ubora wao kuanzia mashinani ni miongoni mwa hatua ambayo ni faida kuu ya utaratibu wa ufanisi wa mchezo huu nchini kwa jumla.