Uhuru, Gachagua waungane kumzima Ruto Mlima Kenya
RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta anastahili kuungana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya linatoa mwaniaji wa urais mnamo 2027 na kumpeleka Rais William Ruto nyumbani.
Kwenye uchaguzi wa 2022, eneo la Mlima Kenya lilionyesha uaminifu mkubwa kwa Rais Ruto na kumpigia kura licha ya kuwa kiongozi wao mkuu wakati huo, Bw Kenyatta alikuwa akimuunga mkono Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Wapigakura wa mlimani walimpa Rais Ruto asilimia 87 za kura na kwenye idadi ya kura milioni 7.1 ambazo Rais alijizolea, karibu milioni nne zilitoka kwenye kapu lao.
Ni wakati ambapo viongozi na wakazi wa Mlima Kenya wanastahili kuthamini idadi ya kura ambazo wanazo na kuzitumia aidha kuingia serikalini au kuingia katika miungano baada ya uchaguzi mkuu.
Kati ya sababu ambazo zilimsaidia Bw Kenyatta kuingia mamlakani mnamo 2013, ni idadi ya kura za Mlima Kenya na Bonde la Ufa, ambapo jamii kutoka maeneo hayo mawili zilithamini na kututumia idadi yao vyema.
Wakati huo, Rais Kibaki ambaye pia alikuwa akitokea mlimani alikuwa akikamilisha muhula wake na wengi walitarajia kuwa ingekuwa vigumu sana kwa rais mpya kutoka ukanda huo.
Kwa kipindi kimoja, Bw Kenyatta alitupilia mbali azma yake na kukubali kumuunga mkono Musalia Mudavadi japo wajumbe wa TNA baadaye walimkabili, wakamkataza na kusema liwalo na liwe lazima asimame.
Kilichofanya Bw Kenyatta awanie urais wakati huo badala ya kuwa naibu wa Dkt Ruto, ni kwa sababu takwimu zilionyesha kuwa alikuwa na kura nyingi kutoka ngome yake ya kisiasa kumliko.
Ushirikiano wa wawili hao ulihakikisha kuwa wanapata ushindi kwa kuzoa kura kutoka Bonde la Ufa na Mlima Kenya na kumbwaga waziri mkuu wa wakati huo, Bw Odinga.
Kutokana na tukio lililoshuhudiwa Embu wikendi iliyopita ambapo wananchi waliwachangamkia Uhuru na Gachagua, wakati umetimia ambapo wanasisa hao wawili wanastahili kuhakikisha kuwa jamii hiyo inatumia idadi yake ya kwa manufaa yao kisiasa.
Jamii haiwezi kuwa na zaidi ya kura milioni nne kisha inahangaishwa na hata kigogo wao wa kisiasa kuondolewa kimadharau jinsi ambavyo Bw Gachagua alivyofanyiwa mwezi uliopita.
Ukweli ni kuwa kwa sasa, Mlima Kenya upo kwenye upinzani kwa sababu ya makosa waliyoyafanya 2022, ambapo waliingia kwenye ushirikiano na Rais Ruto bila chama chochote cha kisiasa.
Mabw Kenyatta na Bw Gachagua wanastahili kusaka chama kingine cha kisiasa kwa sababu ni dhahiri kuwa kwa sasa wakazi wa Mlima Kenya hawako UDA.
Kuwa na chama cha kisiasa kutahakikisha kuwa eneo hilo linapata wabunge wao ambao hawatashawishiwa na watu wa vyama vingine ikifika wakati wa kumpiga vita nyapara wao wa kisiasa.
Afadhali Mlima Kenya uwe na mwaniaji wa urais ambaye hata akianguka debeni, anaweza kutumia idadi ya kura na wabunge wake kuingia kwenye muungano na mshindi.
Hali hii itakuwa afadhali kuliko kumuunga mwaniaji kutoka nje ya eneo hilo kisha akishinda tofauti za kisiasa zinazuka na anaishia kwenye kijibaridi cha kisiasa kama Bw Gachagua.