Maoni

Vijana kuandaa maandamano bila Raila kwafaa kumkosesha usingizi Ruto

Na DOUGLAS MUTUA July 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MOJAWAPO wa mambo ambayo huenda yanamkosesha usingizi Rais William Ruto ni kwamba sasa ni bayana Wakenya wanaweza kuandaa maandamano bila kuongozwa na kinara wa siasa za Upinzani, Bw Raila Odinga.

Katika masuala ya kisiasa, na hata ya kijeshi, mambo huwa rahisi unapokabiliana na adui unayemjua. Akili huzugika kikweli unapopata vipigo kutoka kwa watu usiowajua kwa sababu kamwe huwezi kuelezwa mbinu zao.

Huwezi kabisa kufahamu zinakotoka nguvu zao, wala tabia zao za kawaida katika mambo ya makabiliano huna mwao nazo, hivyo hukosi kujikuna kichwa mara kadha au kukosa usingizi ukiwaza na kuwazua.

Nadhani hiki ni kipindi kigumu mno kwa Dkt Ruto kuwa kiongozi wa nchi kwa kuwa hawezi kutumia mbinu ambazo tangu mwanzo zimetumiwa na watangulizi wake kumdhibiti Bw Odinga.

Na ni aibu kuwa amiri mkuu wa majeshi ya ulinzi na pia kinara wa majasusi wasiokuwa na habari kwamba maandamano hayo yanayoandaliwa na kizazi kichanga, almaarufu Gen Z, yangetokea.

Huenda kwetu hili ni suala la kiuchumi, wananchi na akili zao kukataa kunyanyaswa na serikali waliyojichagulia wenyewe, lakini kwa Dkt Ruto ni suala la usalama wa taifa.

Naam, kwa kuwa tangu nchi hii iwe huru hatujawahi kuwaona waandamanaji wakiingia bungeni na kuliwasha moto jengo lenyewe, na kana kwamba tendo hilo halikutosha, wakachoma na ofisi za Jimbo la Nairobi.

Je, wajuaji wa Gen Z wangepanga mabaya zaidi? Unakumbuka kaulimbiu ya maandamano ya Alhamisi iliyopita ilikuwa gani? Eti kuitwaa na kuikalia Ikulu!

Japo vijana hao hawakufanikiwa kufanya hivyo Nairobi, naambiwa Ikulu ndogo ya Nakuru inajua sura zao kwa maana waliziwasilisha pale si tu ‘kuwasalimu’ wenyeji bali pia kumtahadharisha kiongozi wa nchi kwamba kwake kunaweza kuingiwa.

Wabunge waliochomewa makwao na wengine walioingia baridi wakachapisha fulana za kuomba msamaha, baadhi yao wakanywea na kujificha nyumbani kwao wasionekane na kufanyiwa mambo wanajua hali imebadilika.

Wewe huoni ajabu kwamba siku zote hizi wanasiasa, baadhi yao vijana wachanga sana, wamekuwa wakimtukana Bw Odinga ila hawajawahi kujifungia nyumbani kwa kumwogopa?

Huoni ajabu kuwa wanasiasa – ambao tangu hapo wakipawa fursa za kwanza kuwahutubia waumini makanisani – wamenywea hivi kwamba hawawezi kuthubutu kwenda makanisani?

Ajabu iliyoje kwamba wahubiri hawawezi kuwaalika wanasiasa kwenye michango isiyoisha kanisani kwa kuwa huenda kukazuka vurumai vijana wa Gen Z wakiamua kufika pale kutoa ‘salamu’!

Wahubiri wenyewe wamezindukana ghafla wakaelewa kuwa ndoa kati yao na serikali ni haramu,

Niliwahi kuandika kwenye magazeti haya, mara tu baada ya Bw Odinga kupokezana mkono wa maridhiano na aliyekuwa rais, Bw Uhuru Kenyatta, kwamba ni sharti Wakenya wazue mbinu za kujipigania badala ya kumtegemea Bw Odinga pekee.

Kwamba hilo limefanyika machoni petu, tena haraka sana, ni jambo linalopaswa kutupa matumaini, si kutuhuzunisha. Tungeendelea kumtegemea Bw Odinga, labda tungeishia kuwa mazuzu wa kisiasa kama Watanzania, watu wasiotishia serikali ikawasikiliza!

Gen Z ni kizazi cha kuvuliwa kofia, si kulaaniwa, kwa sababu kimeipa nchi yetu matumaini ya kuendelea kupigania haki za kimsingi ambazo ziliwakosesha mababu zetu hata lepe la usingizi.

Hata hivyo, uzalendo unapaswa kuwa msukumo wa pekee wa kizazi hicho. Nasema hivi kwa kuwa naelewa fika kwamba watu waovu, wanasiasa au vinginevyo, wanaweza kutumia fursa hii ya maandamano kuwateka akili vijana wetu. Hebu na Gen Z iwe macho!

Serikali nayo, hata baada ya kupata fedheha ya mwaka kwa majasusi wake kulala usingizi wa pono kazini, inapaswa kujizoazoa na kuwapa mafunzo mapya majasusi hao, waache kuketi kwenye baa wakirekodi umbea wa walevi!

Na isisahau kuyashughulikia ambyo yaliyowakasirisha mno Gen Z; kuyapuuza ni kuahirisha maafa, yaje kutokea siku za usoni.

[email protected]